Ajali za bodaboda zilivyoua watu 8,000 kwa miaka 10

Monday April 22 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Jumla wa watu 8,004 wamefariki dunia kutokana na ajali za pikipiki huku 35,231 wakijeruhiwa katika kipindi cha miaka 10, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limeeleza.

Takwimu hizo zinatajwa wakati kukiwa na ongezeko la pikipiki zinazoingia nchini kwani kati ya vyombo vya moto milioni 2.1 vilivyosajiliwa mwaka 2018, milioni 1.3 ni pikipiki.

Akitoa takwimu hizo hivi karibuni, Kamanda wa Kikosi cha Polisi, Usalama Barabarani (SACP), Fortunatus Muslimu alisema idadi hiyo imetokana na rekodi ambazo zilichukuliwa na jeshi hilo kuanzia 2009 hadi 2018.

Alisema takwimu hizo zinaonyesha madhara makubwa yanayotokana na ajali za bodaboda ambazo zimesababisha watu wengi kufariki dunia, kujeruhiwa na kubaki na ulemavu wa maisha.

“Jumla ya ajali kwa kipindi cha miaka 10 zilizosababishwa na pikipiki zilifikia 37,421 ambazo zilisababisha majeruhi 35,231 na vifo 8,004,” alisema Muslimu.

Alisema kupungua kwa ajali kuanzia mwaka 2016 hadi 2018, kumesababishwa na operesheni za ‘kamata viroba na nyakua nyakua.’

Advertisement

“Kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, ajali za barabarani zimepungua kwa kiasi kikubwa, ajali zilizohusisha bodaboda zimepungua kutoka 2,128 mwaka 2016 hadi kufikia 694 kwa mwaka 2018,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba takwimu zinaonyesha kuendelea kupungua kwa ajali, vifo na majeruhi, lakini watu ambao wanafariki dunia na kujeruhiwa bila kutolewa taarifa kutokana na ajali za bodaboda bado idadi yao ni kubwa.

Mrakibu Msaidizi na Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Deus Sokoni alisema ajali za bodaboda zimekuwa adha hata kwa waenda kwa miguu ambao wengi wanajeruhiwa na kufariki dunia.

“Katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, waenda kwa miguu 467 wamefariki dunia baada ya kugongwa na bodaboda,” alisema.

Aidha, ajali za bodaboda zimekuwa zikiigharimu Serikali katika matibabu. Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya majeruhi 22,836 waliofanyiwa upasuaji kitengo cha dharura Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) mwaka 2015-2018, asilimia 70 walikuwa ni majeruhi wa bodaboda.

Daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa na maradhi yasababishwayo na ajali MOI, Kennedy Nchimbi alisema idadi ya majeruhi kwa mwaka 2015/16 ilikuwa 7,884 na mwaka 2016/17 ilipungua na kufikia 6,669 na mwaka 2017/18 iliongezeka hadi kufikia 8,283 na kufanya jumla ya wagonjwa waliohudumiwa kufikia 22,836 na kwamba asilimia 70 walikuwa wa ajali za bodaboda.

Alisema kwa kuwa pikipiki ni chombo kilicho wazi, ni rahisi abiria kuumia mguu, kiuno, kifua na maeneo mengine ya mwili na kwamba yanayoumia vibaya ni kichwani kutokana na kutovaa helmeti.

“Asilimia karibu 40 ya wagonjwa wanaofika hapa (MOI) ripoti zinaonyesha hakuwa wamevaa helmeti, mwingine alilifunga nyuma au hana kabisa, wakati mwingine zinavaliwa si kwa usahihi, wapo wanaokwepa kuzivaa kutokana na staili za nywele,” alisema Dk Nchimbi.

Licha ya ongezeko hilo, bado MOI inaelemewa na gharama kubwa za kuwahudumia wagonjwa wa ajali kwani wengi wao hawana ndugu.

Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi alisema matibabu ya wagonjwa hao huchukua muda mrefu, “wapo waliokuja mjini kutafuta maisha, ndugu zao hawapo kwa hiyo wanapopata ajali na kulazwa wodini hawa wanahudumiwa na taasisi kuanzia matibabu yao, mavazi na chakula.

“Huwa tunawatangaza kwenye vyombo vya habari na ikitokea bahati mbaya wakafariki, ikiwa ndugu zake hawajapatikana tutafanya taratibu zingine na mochwari ambako mwili unatakiwa ukae kwa muda fulani na wale watawasiliana na manispaa ambao watazika.”

Advertisement