Ajikata tumbo, avuta utumbo nje akitaka kujiua

Muktasari:

Mkombozi Bakari (32),  mkazi wa kata ya Kwamagome halmashauri ya mji wa Handeni mkoani Tanga amenusurika kifo baada ya kujichoma kisu tumboni na kuvuta utumbo wake nje

Handeni. Mkombozi Bakari (32), mkazi wa kata ya Kwamagome halmashauri ya mji wa Handeni mkoani Tanga amenusurika kifo baada ya kujichoma kisu tumboni, kuvuta utumbo wake nje.

Bakari ambaye aliokolewa na ndugu zake alitaka kujiua kutokana na kutafutwa na Jeshi la Polisi akituhumiwa kumuua mama mkwe wake.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Machi 23, 2019, kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe amesema, “Ni kweli alitaka kujiua, huyu mtu alifanya tukio la mauaji, amemuua mama wa mke wake kutokana na ugomvi wa kifamilia, alimchoma na kitu cha ncha kali.”

“Kipindi wananchi wanampeleka kituo cha polisi, akatumia kisu kile kile kujichoma tumboni na kuutoa utumbo wake, bahati nzuri walimuwahi wakamuwahisha hospitalini na sasa anaendelea na matibabu na akitoka anaendelea na mashtaka yake.”

Akisimulia tukio hilo ndugu wa Bakari, Rajabu Magao amelieleza Mwananchi kuwa ndugu yake huyo alikuwa akitafutwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mauaji ya mama mkwe wake baada ya kumchoma kisu kifuani.

“Mama mkwe wake alifariki dunia Machi 21, 2019  na yeye (Mkombozi) alikimbia kusikojulikana. Siku moja baadaye alionekana na wananchi walitambua alipo, walipokwenda kumkamata alichomoa kisu na kujichoma,” amesema Magao.

Magao amedai ndugu yake huyo alichukua uamuzi huo kutokana na ugomvi wa kifamilia, ikielezwa kuwa hakuwa na maelewano na mkewe.

Muuguzi wa zamu hospitali ya wilaya ya Handeni, Monica Amiri amesema walimpokea Bakari akiwa na jeraha kubwa tumboni na moja kwa moja alipelekwa chumba cha upasuaji.

“Jeraha lilikuwa kubwa ila baada ya kumchunguza tukaona hakupata madhara makubwa, anaendelea na tiba kwa sasa,” amesema Monica.