Ajira za Muungano zaundiwa mkakati

Waziri  wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano (Mazingira), January Makamba akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo

Muktasari:

Serikali yakiri ajira za Muungano bado ni shida kwa upande mmoja wa Muungano, waamua ofisi ya utumishi ijengwe Zanzibar


Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, January Makamba amekiri kwamba Serikali haijafanya vizuri katika suala la utumishi kwenye uwiano wa Muungano.

Makamba amesema kumekuwa na shida katika kuweka uwiano huo na ndiyo maana kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu.

Alikuwa anajibu swali la Mbunge wa Welezo, Saada Mkuya (CCM) bungeni mjini Dodoma leo Ijumaa, Februari 1.

Mkuya ametaka kujua ni ajira ngapi zinapatikana kwa Wazanzibar kupitia makubaliano ya kutatua kero za Muungano.

Waziri amesema Serikali ilishaona mapungufu hayo na kuamua kuyafanyia kazi na wameomba ofisi ya utumishi ijengwe Zanzibar ambako vijana wanaoomba kazi ndani ya Muungano watafanyiwa usaili huko.

"Lakini niwaombe vijana wa Zanzibar wanaoomba ajira ndani ya Muungano wasiandike anuani za Bara kama ambavyo baadhi hufanya badala ya kuandika anuani za Zanzibar," amesema Makamba.

Hata hivyo Naibu Spika, Tulia Ackson ametahadharisha suala la anuani wakati wa kuomba kazi kuwa linaweza kuleta tafsiri ya Uzanzibar na Ubara ambako nchi ilishatoka.