Al Bashir avunja baraza la mawaziri, ateua wanajeshi

Rais wa  Sudan Omar al-Bashir 

Muktasari:

Rais Al Bashir mbali na kuvunja baraza la mawaziri pia ametangaza hali ya hatari na kuteua wanajeshi kusimamia usalama wa mikoa yote 

Sudan.  Rais wa  Sudan Omar al-Bashir ametangaza hali ya hatari nchini humo kwa kipindi cha mwaka mmoja na pia ameivunja Serikali yote.

Al Bashir pia ameteua maofisa wa  jeshi na maofisa wa usalama kusimamia mikoa yote 18 ya nchi hiyo.

Alitangaza uamuzi huo kupitia Televisheni ya Taifa  huku akitaja majina ya baadhi ya viongozi hao wa jeshi watakaochukua  nafasi za baraza la mawaziri.

Bashir alisema hawezi kubadili  wizara za Ulinzi na  Mambo ya Nje na Sheria.

Kiongozi huyo anayekabiliwa na changamoto ambayo haijawahi kutokea katika miaka 30 ya utawala wake pia hajamteua waziri mkuu mpya mpaka sasa.

Al Bashir pia amelitaka Bunge liahirishe kufanya mabadiliko ya katiba ambayo yangemwezesha kuwania muhula mwingine wa urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Maandamano makubwa ya kupinga Serikali yake yamekuwa yanafanyika katika mji mkuu Khartoum na miji mingine kumtaka Rais huyo ajiuzulu. Maandamano hayo yalianza kwa kupinga kupandishwa bei za bidhaa kadhaa.

Mapema Kitengo cha Usalama wa cha Taifa (NISS) kilisema kwamba kiongozi huyo anatakiwa kuachia madaraka mara moja.

Wananchi wameandamana kwa mfululizo wakishinikiza kung’atuka kwa kiongozi huyo lakini wamekuwa wakikabiliana na polisi waliokuwa wanatumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Akiwa kwenye televisheni hiyo alisema ‘’Natangaza hali ya dharura nchini kote kwa mwaka mmoja," alisema.

“Pia natangaza kuifuta  Serikali katika ngazi ya shirikisho na ngazi za mkoa."

Zaidi ya watu 1,000 wanashikiliwa na polisi tangu yalipoanza maandamano ya kumpinga rais huyo huku zaidi ya watu wengine 40 wakipoteza maisha kwa kushambuliwa na vyombo vya usalama.

Rais Bashir (75) ameitawala nchi hiyo kwa muda mrefu  baada ya kushinda mara kwa mara tangu alipochaguliwa kuwa Rais mwaka 1989.