VIDEO: Alichokisema Bashe mbele ya Magufuli

Muktasari:

Hussein Bashe leo Jumatatu ameapishwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Ikulu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania huku akisema anakwenda kutekeleza yale aliyokuwa akiyasoma na kuyasikia ndani ya Bunge.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema atajitahidi kuhakikisha anatimiza yaliyo ndani ya mamlaka atakayopewa ili kulisukuma gurudumu la maendeleo mbele.

Bashe ameyasema hayo leo Jumatatu Julai 22, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam waati akitoa salamu zake baada ya kuapishwa na Rais wa Tanzania, John  Magufuli kushika wadhifa huo.

Amesema anafahamu sekta ya kilimo, anafahamu changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa kuzisoma katika makaratasi na taarifa zinazopelekwa ndani ya Bunge na sasa atakwenda kuziona katika uhalisia.

“Binafsi nafahamu sekta ya kilimo ilivyoajiri asilimia 65 hadi 70 ya wanyonge na wakati mwingine kimekuwa kikiitwa kilimo cha kujikimu, kilimo ni maisha, biashara,” amesema Mbunge huyo wa Nzega Mjini

“Na nchi hii kuelekea uchumi wa viwanda ni lazima tuwajengee uwezo wakulima, hivyo nikuahidi (Rais Magufuli) sitakuangusha kwa kadri ya uwezo wangu, nitajitahidi kutimiza majukumu yangu kwa uwezo wa mwenyezi Mungu,” amesema Bashe

Bashe aliteuliwa jana Jumapili na Rais Magufuli kushika wadhifa huo kuchukua nafasi ya Innocent Bashungwa ambaye alikwisha kuteuliwa kuwa waziri wa viwanda na biashara.