Alichokisema Dk Tulia kuhusu mbunge CCM kuchana hotuba ya upinzani

Wednesday June 19 2019

Mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Vuma

Mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Vuma aliyechana hotuba ya bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mwaka 2019/2020 jana Jumanne Juni 18, 2019 katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020, 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema wabunge wa upinzani ambao hawajaridhishwa na uamuzi wake kuhusu mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Vuma aliyechana hotuba ya bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mwaka 2019/2020,  waandike barua kwa katibu wa Bunge kwa mujibu wa kanuni za chombo hicho cha kutunga sheria.

Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 19, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu mwongozo wa kaimu mnadhimu wa kambi hiyo, Joseph Selasini aliyetaka Vuma kuomba radhi na kupelekwa katika kamati ya maadili ya Bunge.

Katika ufafanuzi wake, Dk Tulia amesema Vuma hawezi kupelekwa katika kamati hiyo kwa kuwa kipindi cha nyuma mbunge wa Bunda (Chadema), Ester Bulaya aliwahi kurusha vitabu bungeni na kuvichana lakini hakupelekwa katika kamati hiyo.

Jana jioni Jumanne Juni 18, 2019 wakati wa mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020, Vuma  alichana kitabu hicho na kusema kina maneno yasiyofaa na kinafaa kuchanwa na kisha kukichana.

Kitendo hicho kilisababisha zogo bungeni na mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka kutoa taarifa akitaka Vuma kuomba radhi, na Dk Tulia kumtaka mbunge huyo kufanya hivyo kwa kauli aliyoitoa wakati akichana kitabu husika, si kwa kitendo chake cha kukichana.

Uamuzi huo haukuwapendeza wabunge wa upinzani na kulalamikia jambo hilo kitendo kilichosababisha Dk Tulia kuwatoa nje ya ukumbi wa Bunge wabunge wa Chadema, Esther Matiko (Tarime Mjini), John Heche (Tarime Vijijini) na Dk Emmaculate Sware (Viti maalum).

Advertisement

Katika ufafanuzi wake wa leo kuhusu mwongozo wa Selasini, Dk Tulia amesema, “Ikiwa kuna maamuzi ambayo yametolewa na kiti ambayo mbunge hakubaliani nayo,  kanuni ya 5 (4) inatutaka tuandike kwa katibu wa Bunge na Spika ataitisha kikao mahsusi kwa ajili ya kazi hiyo. Uamuzi ukitolewa na kiti mbunge hawezi kuhoji tena.”

Alichokisema Selasini

“Mjadala utakaoendelea hivi punde utahusu hotuba ya bajeti ya fedha, maoni ya kamati ya bajeti na kambi rasmi ya upinzani bungeni. Jana tulishuhudia Vuma akichana kitabu cha maoni ya upinzani.”

“Maoni yanayoletwa bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 99 (9) na kufanya kuwa kumbukumbu rasmi za Bunge,” amesema Selasini akibainisha kuwa wabunge wa upinzani wana hasira kwa kitendo hicho.

Amesema naibu Spika wakati akitoa uamuzi wa suala hilo alisema hakuna kanuni inazuia mbunge kuchana kitabu bungeni, “Kama ambavyo hakuna kanuni inayoeleza mbunge akijisaidia bungeni anafanywa nini. Kumbe kuna mambo yanapaswa kuongozwa kwa busara ya kiti chako.”

Selasini amesema ili kuwe na mjadala wa amani, alitaka kiti kimtake Vuma kuomba radhi na kuagiza apelekwe katika kamati ya Bunge ya maadili ili jambo hilo kutojirudia.

“Leo imechanwa hotuba ya upinzani lakini inaweza kutokea mbunge yoyote akasimama na kuchana hotuba ya waziri. Hili ni Bunge linatizamwa na watu na dunia kwa ujumla,” amesema Selasini.

Ufafanuzi wa Dk Tulia

Katika maelezo yake Dk Tulia amesema, “Siku zote kiti huwataka wabunge kuwa na subira na kuheshimiana humu ndani wote tunakubaliana lakini wakati wa utekelezaji kunakuwa na changamoto. Wakati mwingine uamuzi unapotolewa na kiti (mbunge) hupata hisia kuwa ameonewa kwa kusahau kwamba jambo hilo pengine yeye au mwenzake ameshalifanya na kiti kikafanya uamuzi unaofanana na hayo.”

“Siku moja nikiwa nimekaa hapa mbele kambi ya upinzani niliilelekeza itoke nje na Bulaya akabeba vitabu na kuvirusha humu ndani vikachanika.”

 

Dk Tulia amesema Bulaya hakuadhibiwa kwa sababu ya vitabu, kubainisha kuwa yaliyotokea jana Vuma alipaswa kuondoa maneno yake aliyozungumza wakati akichana kitabu hicho.

 

“Uamuzi unaotolewa na kiti unatolewa kwa kuangalia pande zote mbili, kama ambavyo Bulaya hakupelekwa katika kamati ya maadili hata Vuma hakupelekwa na hatapelekwa Hakuna anayependelewa kwa sababu hakuna mbunge ambaye ni mkubwa kuliko mwingine,” amesema Dk Tulia.

Advertisement