VIDEO: Alichokisema IGP Sirro mbele ya Rais Magufuli kuhusu chaguzi zijazo

Muktasari:

Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa Oktoba mwaka 2019 na uchaguzi mkuu mwaka 2020 ambapo Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro amesema katika kipindi chote cha chaguzi amani itatamalaki.

Dar es Salaam. Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro amemuhakikishia Rais wa nchi hiyo, John Magufuli kuwa vikosi vyake vimejipanga kuhakikisha amani na utulivu vitatawala katika chaguzi zijazo.

IGP Sirro ameyasema hayo leo Jumatatu Julai 15,2019 wakati wa uzinduzi wa nyumba za makazi ya askari yaliyopo eneo la Magogo mkoani Geita.

Amesema viongozi wazuri watachaguliwa kukiwa na Amani na utulivu hivyo watahakikisha hali hiyo inatamalaki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Nakuhakikishia amani itatamalaki na uchaguzi utapita salama. Hatutamvumilia mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuvuruga amani. Sisi vyombo vya dola tuko tutahakikisha tunafuata sheria kuhakikisha wananchi wanaishi salama,” amesema

IGP Sirro amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwezesha kujengwa kwa nyumba hizo ambazo zinakwenda kutatua changamoto ya makazi ya askari.

Kuhusu mauaji ya Watanzania tisa yaliyotokea nchini Musumbiji hivi karibuni, IGP Sirro amesema watu watano wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo wanashikiliwa kwa uchunguzi.