Alichokisema Matiko baada ya Spika Ndugai kumtoa nje bungeni

Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko akitoka kwenye ukumbi wa Bunge baada kuamriwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kutoka ukumbini kufuatia kupiga kelele wakati spika alipokuwa akitangaza madeni aliyonayo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko amesema kama mabenki hutoa mikopo kwa wateja wake na kutoiweka wazi, hata Spika Job Ndugai hakupaswa kueleza hadharani fedha anazodaiwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema


Dodoma.  Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko amesema uamuzi wa Spika Job Ndugai kumtoa nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kupinga kauli ya kiongozi huyo kutaja kiwango cha fedha anazodaiwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema si sahihi.

Akizungumza na Mwananchi nje ya viwanja vya Bunge leo Jumatano Aprili 3, 2019, Matiko amesema hata mabenki nchini Tanzania hayatoi siri za wateja waliokopa fedha, kuhoji sababu za Ndugai kutaja fedha anazodaiwa Lema.

Leo Ndugai wakati akieza bungeni kuwa kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itamhoji Lema saa 8 mchana kutokana na kauli yake aliyoitoa jana bungeni kuwa Bunge ni dhaifu, aligusia deni analodaiwa mbunge huyo.

Wakati akieleza kuhusu deni hilo, wabunge wa Chadema walikuwa wakizungumza na Ndugai alisikika akimtaka Matiko kuchukua vitu vyake na kutoka nje, amri ambayo ilitekelezwa na mbunge huyo ambaye pia ni mhazini wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha).

“Nafikiri kiubinadamu kuna mambo hata katika benki ukienda hawatoi siri za mteja hata ukikopa mabilioni ili mradi tu umekubalika kukopa,” amesema Matiko.

“Haikuwa sawa, hata kama Lema wameamua kumudhibu na kumpeleka katika kamati kwa aliyoyasema jana iwe hivyo lakini si kuweka wazi mambo yake, ila Spika ameamua kunitoa sawa tu.”

Akizungumzia madeni ya Lema Ndugai amesema, “Yapo mambo ambayo hawasemi wacha tuseme kidogo (Lema) amekopa Sh 644 milioni.  Sasa hivi ameshalipa zimefika Sh419 milioni huu ni msongo wa mawazo ndio maana anafika mahali anajilipua tu nakadhalika.”

Jana, Lema wakati akizungumza bungeni baada ya kamati ya Haki, Maadili ya Madaraka ya Bunge kupendekeza mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kusimamishwa na Bunge kuhudhuria mikutano miwili ya chombo hicho, aliungana mkono kauli ya Mdee aliyetiwa hatiani kwa kusema Bunge ni dhaifu.

Kufuatia kauli hiyo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson aliiagiza kamati hiyo kumhoji Lema, akimtaka athibitishe ukweli kuwa Bunge ni dhaifu.