VIDEO: Alichokisema Mbunge CCM mwaka 2018 chaibuka mitandaoni

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Video ya mwaka 2018 inayosambaa mitandaoni ikimuonyesha mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba akizungumza katika kikao cha Bunge la Bajeti na kukosoa takwimu na ukuaji wa deni la Taifa, uwekezaji na kodi imeibua mjadala mitandaoni na kuonekana kama ni jambo alilolizungumza katika Bunge la bajeti mwaka 2019/2020 linaloendelea jijini Dodoma.


Dodoma. Unaweza kusema kati ya mijadala inayotikisa kwenye mitandao ya kijamii leo Ijumaa Juni 7, 2019 ni mchango wa mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba alioutoa katika Bunge la bajeti la mwaka 2018/2019.

Video inayomuonyesha mbunge huyo akizungumza katika chombo hicho cha kutunga sheria ilianza kusambaa mitandaoni jana usiku na kuonekana kama ni jambo alilolizungumza katika vikao vya Bunge la bajeti mwaka 2019/2020 linaloendelea jijini Dodoma.

Serukamba alianza kuchambua deni la Taifa akitumia neno ‘copy and paste’,  kwamba Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa ikirudia takwimu za deni hilo, kuhoji Serikali kutaka kufanya kila jambo na kutoamini sekta binafsi na kukosoa  ukusanyaji wa kodi bila kueleza hali ilivyo katika uzalishaji.

Alichokisema

“Nimekuja na mipango mitatu wa 2016/2017, 2017/ 2018 na 2018/2019 naanza na deni la Taifa. Kwenye mpango wa 2016/17 tuliambiwa ilipofika Oktoba 2015 deni la Taifa lilikuwa Dola 19 bilioni ikilinganishwa na dola bilioni 18 za Oktoba 2014.”

“Lakini tulivyokuja mpango wa 2017/18 tukaambiwa deni la Taifa limekuwa dola 18 bilioni ongezeko la asilimia 9.76, sasa mwaka uliopita ilikuwa dola 19 bilioni mwaka unaofuata tunaambiwa dola 18 bilioni  lakini kuna ongezeko,” amesema Serukamba.

“Hawakuishia hapo wanasema ongezeko hili wanalinganisha na dola 16 bilioni za 2015. Kwenye mpango huu wa mwanzo wanasema Oktoba ilikuwa dola 19 bilioni, kwenye mpango huu wa pili wanasema Oktoba ilikuwa dola 16 bilioni na kwenye mpango huu mpya wanasema deni la Taifa limefika dola 26 bilioni ukilinganisha na dola 22 bilioni za Juni 2016.”

Amesema, “Lakini kwenye ripoti ya June tunaambiwa ni  dola 19 bilioni.  Moja ya tatizo ni takwimu zinazoletwa na Wizara ya Fedha haiwezekani tukawa na makosa zaidi ya dola 3 bilioni. Maana yake ukiangalia mipango yote mitatu ni copy and paste, ukipitia yote kinachosemwa ni kile kile.”

Amesema kuna mambo yanapangwa lakini kinachofanyika hata Bunge halijui, “Deni la Taifa linapanda kwa Sh4 trilioni kwa mwaka kulingana na ripoti ya BoT (Benki Kuu ya Tanzania) maana yake tumeamua kila kitu kinafanywa na serikali, hatuwezi kuendelea.”

Mbunge huyo amesema hakuna Taifa duniani ambalo kila kitu kinafanywa kwa fedha zake, kusisitiza kuwa hata kama ni mkopo bado unabaki kuwa wa Serikali husika.

“Mwenyekiti (wa Bunge) wewe shahidi uwanja wa ndege wa Moscow International umejengwa na mtu. Humu ndani tunasema tutafanya PPP (Sekta Umma na Sekta Binafsi) lakini ukitafuta miradi ya PPP haipo na Serikali hii haiamini katika sekta binafsi.”

“Bunge hili tukubaliane Waziri wa Fedha atuambie Serikali hii haikubaliani na sekta binafsi kwa sababu mipango yako mwanzo mpaka mwisho huongelei sekta binafsi, kama tumerudi katika ujamaa tuambie tujue lakini haiwezekani tuimbe ujamaa na kutaka matokeo ya kibepari,” amesema Serukamba.

Akizungumzia moja kati ya mipango hiyo mitatu aliyokuwa akiizungumzia,  Serukamba amesema haukuwa ukizungumzia usalishaji, kukuza tija katika mazao.

“Nilitarajia wangesema tumezalisha tani hizi za mahindi mwaka kesho tutazalisha tani kiasi fulani lakini hakuna kitu. Hakuna pamba, kahawa, korosho sasa tunapanga nini.”

“Huku wanasema wataweka fedha TIB (Benki ya uwekezaji Tanzania) zisaidie miradi lakini tangu wameanza kusema hawajaweka hata shilingi moja. Mambo ambayo mnajua hamuwezi kuyafanya msiandike. Hatuongelei uzalishaji sisi tunahangaika kubana. Mmegeuza uchumi wa kubana. Tunaleta sheria ya kubana hakuna anayeongelea kupanua,” amesema Serukamba.

Mbunge huyo pia aligusia zao la pamba, "Unaweza kuanzisha kiwanda cha pamba una marobota 240,000 kweli wakati, Bangladeshi kiwanda kimoja kinatumia marobota milioni tano,  hivi tunamdanganya nani?”

“Ninamuonea huruma sana Rais anahangaika ila wenzake hawamuelezi ukweli mtanisamehe. Leo Rais  anasema viwanda vizalishe sukari lakini tumesema siku zote bungeni hakuna aliyetuelewa ila kwa kuwa rais kasema viwanda vitazalisha sasa.”

Kuhusu ukusanyaji wa kodi alisema, “Humu ndani Waziri anaongelea kukusanya kodi peke yake sio kukuza biashara, tunakusanya kodi kwa nani? Leo mabenki yanakufa na uchumi unaofanya vizuri huwa unaangalia mambo mawili; utendaji wa benki na soko la hisa.”

“Nenda Dar es Salaam mauzo ya soko la hisa yameshuka kutoka Sh20 bilioni mpaka Sh2 bilioni na hakuna anayesema. Waziri wa Fedha hasemi na sioni anayejali hili jambo ni nini hii? Hii nchi yetu wote. Haiwezekani viwanja vya ndege, reli, umeme na barabara tujenge kwa pesa yetu sisi ni nani dunia yote imekwenda katika sekta za binafsi.”