Alichokisema Ndugai kuhusu Lissu, ukomo wa mtu kuwa mbunge

Spika Job Ndugai 

Muktasari:

Baada ya Spika Job Ndugai kumtaka mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kurejea nyumbani kwa kuwa hana kibali cha kuwa nje ya nchi, Mwananchi limekuchambulia kifungu cha 71 (1) cha Katiba kinachoeleza ukomo wa mtu kuwa mbunge


Dar es Salaam. Baada ya Spika Job Ndugai kumtaka mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kurejea nyumbani kwa kuwa hana kibali cha kuwa nje ya nchi, Mwananchi limekuchambulia kifungu cha 71 (1) cha Katiba kinachoeleza ukomo wa mtu kuwa mbunge.

Ndugai alitoa kauli hiyo Januari 19, 2019 baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu madai ya Lissu yaliyopo katika waraka wake alioupa jina la ‘Baada ya risasi kushindwa, sasa wanataka kunivua ubunge’.

“Yeye ametoka kuugua aache uzushi arudi nyumbani, tunamsubiri nyumbani. Kitu muhimu ni kwamba ajue hana ruhusa ya Spika ya kuwa huko anakozurura. Sasa achunge kidogo, maana Spika ana nguvu zake, asimpe sababu,” amesema Ndugai.

Katika waraka huo Lissu alieleza kuwa kuna mkakati wa kumvua ubunge kwa kigezo cha utoro bungeni na kueleza kuwa jambo hilo si kweli kwa maelezo kuwa taarifa za kuumwa kwake zipo wazi.

Lissu alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D, mjini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge.

Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyo hiyo usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Alipata matibabu katika hospitali hiyo hadi Januari 6, mwaka jana alipohamishiwa Ubelgiji alikohitimisha matibabu yake Desemba 31, mwaka jana. Mwanasheria huyo wa Chadema ametibiwa kwa jumla ya siku 480 sawa na mwaka mmoja na miezi mitatu na siku 24.

“Nimepata taarifa kutoka kwa watu wawili tofauti kwamba kuna mkakati unaandaliwa wa kunivua ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki,” ameandika Lissu.

“Yaani sijamwandikia katibu wa Bunge taarifa yoyote ya maandishi kuhusu kuumwa kwangu wala matibabu yangu, kwa maneno mengine, sijahudhuria vikao vya Bunge tangu tarehe 7 Septemba 2017 hadi sasa bila sababu au taarifa yoyote rasmi,” alisema Lissu.

Lissu alisema hashangazwi na taarifa hizo, akidai kuwa ni mwendelezo wa chuki na visasi, akieleza kuwa hakuna asiyejua kuwa ni mgonjwa, alishambuliwa akiwa bungeni..

Isemavyo Katiba

Kwa mujibu wa ibara ya 71 (1) inaeleza kuwa mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo;

Ikiwa litatokea jambo lolote ambalo, kama asingekuwa Mbunge lingemfanya asiwe na sifa za uchaguzi au apoteze sifa za uchaguzi au asiweze kuchaguliwa au kuteuliwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii

(b) ikiwa Mbunge huyo atachaguliwa kuwa Rais,

(c) ikiwa mbunge atakosa kuhudhuria vikao vya Mikutano ya Bunge Mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika

(d) ikiwa itathibitishwa kwamba amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma

(e) ikiwa Mbunge ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa Mbunge

(f) iwapo Mbunge anachaguliwa au anateuliwa kuwa Makamu wa Rais.

(g) kwa Mbunge ambaye anatakiwa kutoa taarifa rasmi ya mali kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 70, ikiwa atashindwa kutoa hilo tamko rasmi kwa mujibu wa masharti ya hiyo ibara ya 70 katika muda uliowekwa mahususi kwa ajili hiyo kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, lakini iwapo Mbunge hatakoma kuwa Mbunge kwa mujibu wa jambo lolote kati ya mambo hayo yaliyotajwa na kama hatajiuzulu au kufariki mapema zaidi, basi Mbunge ataendelea kushika madaraka yake kama Mbunge mpaka wakati Bunge litakapovunjwa kwa mujibu wa ibara ya 90, bila ya kuathiri haki na stahili zinazotokana na ubunge wake.