Alichokisema Ndugai kuhusu jengo la Terminal II

Thursday August 1 2019Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema  jengo la pili la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) lilikuwa linatia aibu kwa kuwa lilikuwa dogo na kusababisha mlundikano wa abiria.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Agosti Mosi, 2019 katika uzinduzi wa jengo la tatu la uwanja huo uliofanywa na Rais wa Tanzania, John Magufuli.

“Kawaida duniani mtu akikutembelea anaangalia sebule yako ilivyo, akiona ni chafu anajua nyumba nzima chafu tu, kupitia uwanja huu umetutoa kimasomaso mheshimiwa rais na serikali yako.”

“Wakipita hapa wanapata picha ya Tanzania, kule tulipokuwa ilikuwa ni siri yetu, kulikuwa ni mbanano, hapatoshi na kulikuwa kunatupa aibu sana, kwa niaba ya Bunge tunashukuru,” amesema Ndugai.

Amesema Bunge litazidi kumuunga mkono Rais Magufuli ili kuhakikisha miradi mikubwa inatekelezeka kwa sababu ni historia kubwa inawekwa.

Akizungumzia kuhusu utalii, Ndugai ameitaka Wizara ya Maliasili na Wizara ya Mifugo na Uvuvi  kukaa na kuangalia namna wanavyoweza kutumia utalii wa Pwani ya bahari kuongeza idadi ya watalii.

Advertisement

“Wenzetu nchi jirani wanatumia hifadhi hizi kupata watalii na kwetu haifanyi vizuri kwa sababu iko chini ya Wizara ya Mifugo, hivyo itafutwe namna ya kuboresha sehemu hizi,” amesema Ndugai.

 

 

Advertisement