Alichokisema Profesa Kabudi kuhusu biashara, soko huru SADC

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri SADC, Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza na vyombo  vya habari leo wakati wa mkutano wa Baraza hilo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mwenyekiti mpya wa baraza la mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Profesa Palamagamba Kabudi amesema juhudi za haraka zinahitajika kuongeza kasi ya utekelezaji wa itifaki ya biashara na soko huru la jumuiya hiyo

Dar es Salaam. Mwenyekiti mpya wa baraza la mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Profesa Palamagamba Kabudi amesema juhudi za haraka zinahitajika kuongeza kasi ya utekelezaji wa itifaki ya biashara na soko huru la jumuiya hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Agosti 12, 2019 katika mkutano wa baraza la jumuiya hiyo jijini Dar es Salaam.

Profesa Kabudi amekabidhiwa uenyekiti huo na mtangulizi wake, Netumbo Nandi-Ndaitwah ambaye ni naibu waziri mkuu wa Namibia na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo.

Amebainisha kuwa mkutano huo unafanyika huku kukiwa na msukumo mkubwa wa nje ya jumuiya hiyo unaochagiza kuanzishwa kwa soko la pamoja linalounganisha nchi za jumuiya ya SADC, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).

“Ninaelewa masuala haya yana sekta maalumu za kushughulikia, natambua kazi iliyofanyika katika baraza hili ambalo limekuwa msingi wa kuzalisha mikakati na namna SADC inatakiwa kufanya na kusonga mbele.”

“Ninaamini uamuzi na maelekezo ya mkutano huu yatahakikisha mtangamano wetu haupati athari na mabadiliko ya kidunia, utaendelea kusonga mbele ili kufikia mafanikio,” amesema Profesa Kabudi.