Alichokisema Rais Magufuli ajali ya lori la mafuta Morogoro

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

Rais wa Tanzania John Magufuli ameeleza kushtushwa kwake na ajali ya moto baada ya lori lililokuwa na shehena ya mafuta kupata ajali na kisha kulipuka moto Mjini Morogoro ambapo limesababisha vifo zaidi ya 60 pamoja na majeruhi zaidi ya 70.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu zaidi ya 60 na majeruhi takribani 70 walioungua kwa moto baada ya lori lililokuwa na shehena ya mafuta kupata ajali na kisha kulipuka moto Mjini Morogoro.

Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi Agosti 10, 2019 saa 2 asubuhi ambapo lori hilo lililokuwa linatoka Dar es Salaam limepinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu baada ya dereva wa lori kumkwepa mwendesha pikipiki na kisha mafuta yaliyokuwa yakimwagika kushika moto na kuunguza watu waliokuwa wanayachota.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania, Gerson Msigwa imesema Rais Magufuli ametoa pole kwa familia, ndugu, marafiki na wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hiyo na pia amewaombea majeruhi wapone haraka, huku pia akikemea vitendo vya wananchi wanaovamia magari yenye milipuko akitaka vikomeshwe mara moja.

“Nimeumia sana kusikia idadi kubwa ya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, natoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivi hasa familia za marehemu wote, nawaombea marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka” amesema Rais Magufuli.

“Baadhi ya magari haya yanabeba mafuta ambayo ni hatari kama ilivyotokea Morogoro, yapo magari yanabeba kemikali za sumu, yapo magari yanabeba milipuko nakadhalika, nawaomba sana tuache tabia hii,” amesisitiza kiongozi huyo mkuu

Taarifa hiyo pia imesema, Rais Magufuli amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Steven Kebwe kufikisha salamu zake za pole kwa familia na wote walioguswa na vifo hivyo.

“Rais Magufuli ameagiza wizara zote zinazohusika kushughulikia ajali hii na ametaka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa matibabu ili kuokoa maisha yao,” imesema taarifa hiyo.