Alikiba akubali kumsaidia Diamond tamasha la Wasafi

Wednesday November 7 2018

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Wanamuziki mahasimu nchini Tanzania Alikiba na Diamond Platnumz leo Jumatano Novemba 6, 2018  wameweka historia kwa kukubali kushirikiana katika tamasha la Wasafi linalotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 24, mwaka huu.

Alikiba kupitia mtandao wa Instagram amesema kuwa umesikia ombi la Diamond Platnumz la kutaka kufanya kazi naye katika Tamasha hilo litakaloanza kutimua mkoani Mtwara.

Katika taarifa yake aliyoichapisha kwenye mtandao wa Instagram amesema amelipokea ombi lakini kutokana na kubanwa na majukumu hataweza kushiriki isipokuwa kuwa watamsaidia kwa kumpa udhamini kupitia kinywaji cha Mofaya kitakachoingia sokoni hivi karibuni.

Amesema uongozi wake wa Rockstar Africa upo tayari kuwaunga mkono katika juhudi za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya muziki nchini kwa kutoa udhamini.

“Tumepata salamu zenu, nashukuru kwa mwaliko wenu, ila kwa bahati sitoweza kushiriki kwa sasa kutokana na majukumu ya kuzindua Mofaya katika nchi zingine. Hata hivyo tusingependa kuwaacha hivi hivi, tupo tayari kuwapa udhamini tamasha lenu kupitia kinywaji cha Mofaya.” 

Mwanamuziki Diamond Platnumz alijibu akimshukuru na kusema kuwa mmoja wa viongozi wake, Sallam SK atafanya mawasiliano na Seven.


Advertisement