VIDEO: Aliyejenga nyumba mpaka wa Tanzania na Kenya afunguka

Muktasari:

Umeshawahi kuona nyumba imejengwa katikati ya mpaka wa Tanzania na Kenya. Kama unaona hilo ni jambo geni basi linawezekana na Juma Ally, mmiliki wa nyumba iliyopo katikati ya mpaka huo amesema haoni tatizo licha ya awali kutojua lolote kuhusu mpaka huo.


Tanga. Juma Ally, aliyejenga nyumba katikati ya mpaka Tanzania na Kenya katika kijiji cha Jasini wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga amesema haoni tatizo nyumba yake kuwa eneo hilo.

Amesema nyumba hiyo ipo katikati ya mpaka huo, na baadhi ya vyumba vyake vipo upande wa Tanzania na vingine upande wa Kenya.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 14, 2019 ikiwa ni siku moja baada ya naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Damas Ndumbaro na naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji kutembelea kijiji hicho.

Katika ziara yao hiyo mawaziri hao walikumbana na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na suala la mipaka.

Katika maelezo yake,  Juma amesema  kuwa wao  ni wakazi  wa muda  mrefu  katika  eneo  hilo na hata huduma za kijamii wanazipata kutoka Kenya.

Amesema licha ya kupata huduma hizo Kenya, wao ni Watanzania.

“Nilivyojenga  nilijua nimejenga Tanzania kwa kuwa ni nchi yangu ila baada ya mawaziri  kufika  hapa  ndio nikasikia kuwa  nyumba yangu iko upande wa Kenya na Tanzania,” amesema Juma.