UCHOKOZI WA EDO: Aliyejikata sehemu za siri hastahili mahabusu

Wednesday June 19 2019Edo  Kumwembe

Edo  Kumwembe 

Leo nina habari ya kusikitisha kidogo. Huko kwetu Kusini kuna kijana amejiondoa sehemu yake ya siri akiamini kwamba ilikuwa inamshawishi kufanya uzinzi. Anataka kumrudia Mungu wake. Dunia haitaacha kutuletea watu wanaofanya maajabu. Huyu ni mmojawao.

Polisi wanamshikilia. Sisi tulioishia darasa la saba hatuelewi sana sheria. Anashikiliwa kwa kosa la kutaka kujiua, au inawezekana anashikiliwa kwa hofu kwamba anaweza kuwafanyia wengine kile alichojifanyia.

Wakati mwingine tunaongeza mahabusu au wafungwa katika magereza yetu wakati wenzetu kule majuu wangeweza kuwafanyia kitu tofauti. Mtu aliyejikata sehemu ya siri kwa sababu yoyote ile ujue ana matatizo ya akili. Si mwanadamu wa kawaida.

Huyu anahitaji kukutana na mwanasaikolojia (Psychologist) kuliko kukutana na polisi. Anahitaji maongezi ya muda mrefu na mtu ambaye atasaidia kumrudishia utu wake. Basi! Polisi hakuwezi kumsaidia kitu zaidi ya kuongeza idadi ya mahabusu.

Wapo watu wengi mahabusu na magerezani ambao wametenda makosa ambayo wanaweza kurudia kuyatenda tena kama hawatatibiwa kisaikolojia. Ni kosa ambalo tumeendelea kulifanya kila kukicha kwa sababu tuna tabia ya kutodhibiti kiini cha tatizo.

Huku kwetu wanasaikolojia sio watu muhimu. Hatujui kazi zao. Ulaya ni wanalipwa fedha nyingi kwa ajili ya kurudisha akili za binadamu sawa. Wanasomea kazi hii na wanapewa leseni za kuendesha kazi hizi. Sisi tuko ‘bize’ kutoa leseni kwa waganga wa kienyeji.

Advertisement

Kuna matukio mengi ambayo sio ya kibinadamu yanaendelea nchini kwa sababu watu wamechanganyikiwa na hawana msaada. Wanachukua uamuzi wa ajabu, kuua watoto, wazazi au marafiki. Wote hawa wanapokaribia kuchukua uamuzi huo tunawaona. Tunashindwa namna ya kuwasaidia.

Aliyejikata sehemu za siri ni miongoni mwa watu hawa. Alipaswa kusaidiwa na rafiki zake kabla hajachukua hatua hii, na anapaswa kusaidiwa hata baada ya kuchukua hatua hii. Akili yake haipo kawaida. Maisha ni magumu na yamemchanganya kwa njia moja au nyingine.

Watu wanaopiga fedha sana kupitia watu hawa kwa sasa ni baadhi ya wachungaji. Yamezuka makanisa kama uyoga ambako wamejazana watu wenye matatizo ya kisaikolojia tu. Wanatibiwa katika njia nyingine huku wakitoa sadaka nyingi.

Advertisement