Aliyelipua basi la Dortmund afungwa miaka 14 jela

Muktasari:

Dortmund. Mjerumani huyo alibeti zaidi ya Sh50 milioni akibashiri kuwa hisa za klabu ya Dortmund zingeshuka na akaandaa mpango wa shambulio ili taarifa za tukio hilo zishushe thamani ya hisa na hivyo kujipatia zaidi ya Sh1 bilioni.


Hatimaye raia wa Ujerumani aliyeshambulia kwa bomu basi la Borussia Dortmund mwaka jana ili kushusha thamani ya hisa za klabu hiyo ya soka, hmatengeneze fedha katika hisa za klabu hiyo, amehukumiwa kifungo cha miaka 14 jela.

Mahakama ya Dortmund ilimtia hatiani Mjerumani huyo, Sergej Wenergold, 29, kwa makosa 28 baada ya kulipua mabomu matatu wakati basi likiwa njiani kuelekea kwenye mechi.

Jaji Peter Windgaetter alisema mtu huyo alitegemea watu kuuawa.

Baada ya miezi kumi na moja ya kusikiliza kesi hiyo, Mjerumani huyo ambaye amesomea masuala ya umeme na ambaye amekulia nchini Russia, alipatikana na hatia ya kusababisha mlipuko na makosa mawili ya kusababisha majeraha makubwa. Milipuko hiyo ilimjeruhi beki Mhispania, Marc Bartra na ofisa wa polisi.

Wenergold alikuwa ameishi kwenye hoteli ambayo klabu hiyo imefikia, na akiwa amejificha akalipua mabomu hayo jioni ya Aprili 11, 2017 wakati basi likielekea katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Monaco.

Windgaetter alisema mabomu hayo yalifyatulia baada tu ya basi kuyapita.

Wenergold alificha mabomu hayo ndani ya eneo la hoteli na ambayo kila moja lilikuwa na uzito wa karibu kilo moja, mchanganyiko wa hydrogen peroxide na boriti 65 za ukubwa wa sigara.

Wenergold aliacha barua zinazoeleza kuwa kundi la kigaidi la kiislamu lilihusika na tukio hilo, na hivyo kuzua hofu ya uwezekano wa kutokea shambulizi la kigaidi.

Alikuwa amebeti Euro 26,000 (sawa na zaidi ya Sh54 milioni za Tanzania) akibashiri kuwa hisa za klabu hiyo zingeshuka, na hivyo kuwa na uwezekano wa kujipatia takriban Euro nusu milioni kama mpango huo ungetimia. AFP