Aliyemuua dada yake ahukumiwa kunyongwa

Moshi. Mkazi wa Kijiji cha Tela Magula, Wilaya ya Moshi, Modest Shayo (32) aliyemuua dada yake kisa kila akigombana na mkewe anakimbilia kwa wifi yake huyo, amehukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Hukumu hiyo imetolewa jana na Jaji Patricia Fikirini wa Mahakama Kuu, ambaye aliukataa utetezi wa mshtakiwa kuwa alimuua dada yake, Yasinta Ladislaus kwa sababu ya hasira.

Awali, ilidaiwa na mawakili wa Serikali, Akisa Mhando na Grace Kabu, kuwa Februari 14, 2017 katika kijiji, mshtakiwa alimuua Yasinta kwa makusudi kwa panga.

Siku hiyo saa mbili usiku wakati marehemu yuko jikoni na watoto wake wawili wadogo, alimvamia na kumkatakata kwa mapanga usoni, mikononi na pia kumkata vidole vitatu vya mkono.

Katika utetezi wake, mshtakiwa huyo aliyekuwa akitetewa na mawakili Patricia Eric na Lilian Mushi, alikubali kutenda kosa akisema alifanya hivyo kutokana na ugomvi wa muda mrefu na dada yake.

Alisema dada yake alikuwa akiingilia ugomvi wake na mkewe na siku ya tukio alipata taarifa saa 12 jioni kuwa dada yake amemsafirisha mkewe kurejea kwao.

Katika hukumu yake, Jaji Fikirini alisema ameangalia utetezi wa mshtakiwa na kuona sababu ya kutenda kosa hilo haina mashiko kwani ugomvi alioueleza ulikuwa wa kawaida katika familia.

Jaji Fikirini alisema siku ya tukio, alipata taarifa ya mke wake kusafirishwa saa 12 jioni, lakini akaenda kwa marehemu saa mbili usiku na kwamba muda wote huo alikuwa na muda wa kutosha kutuliza hasira.

Kwa mujibu wa Jaji Fikirini, sababu ya mshitakiwa kwenda nyumbani kwa marehemu masaa mawili baadae ni wazi kwamba mshitakiwa alipanga ni kitu gani anakwenda kumfanyia dada yake huyo.

Jaji Fikirini alisema kwa kuwa upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha shitaka dhidi yake bila kuacha shaka yoyote, anamhukumu mshitakiwa huyo adhabu ya kunyongwa hadi kufa.