Aliyezaa na binti yake, aliyetaka kuua mwanaye watupwa jela

Thursday June 13 2019

 

By Twalad Salum na Babati Chume, Mwananchi

Misungwi/Siha. Mahakama za wilaya ya Misungwi jijini Mwanza na Siha mkoani Kilimanjaro zimewahukumu wazazi kwenda jela kutokana na kukutwa na hatia kwenye makosa yaliyokuwa yakiwakabili dhidi ya watoto wao.

Jacob Shabani (30) mkazi wa Kijiji cha Wanzamiso, Misungwi alihukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kufanya mapenzi na mwanaye wa kuzaa akiwa na umri wa miaka 14 huku Elizabert Mmari (20) akihukumiwa kwenda jela miezi sita baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kumuua kwa sumu mtoto wake wa siku tatu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Misungwi, Erick Marley alitoa hukumu hiyo juzi akisema ameridhishwa na ushahidi wa mashahidi watatu.

Mahakama ilimtia hatiani Shabani na kuuliza kumbukumbu za makosa ya nyuma ambapo alionekana hajawahi kutenda kosa na kuamuru atumikie kifungo cha miaka hiyo 30.

Akitoa ushahidi wake mahakamani hapo mtoto huyo alidai “alinipa ujauzito mara tatu nilizaa mara mbili mtoto mkubwa alifariki mwaka jana kesi ilipokuwa imeanza, mimba moja iliharibika baada ya kunipiga sana, na sasa nina mtoto mdogo ana mwaka mmoja.”

Alidai hali hiyo ilitokea baada ya wazazi kuhitilafiana na mama yake kuondoka nyumbani wakati yeye (mtoto) akiwa na miaka 12 mwaka 2015 na ndipo baba yake aliza kufanya naye mapenzi.

Advertisement

Awali, mwendesha mashitaka wa polisi Ramsoney Salehe akisaidiana na mkaguzi msaidizi wa polisi Juma Kiparo, alimsomea hati ya shitaka la kuzini na maharimu (kufanya mapenzi na mwanae wa kuzaa) kinyume cha sheria ya makosa ya jinai namba 158 (1) (a) sura 16 kama ilivyorejewa mwaka 2002.

Alidai kati ya mwaka 2015 wakiwa huko kijiji cha Mwalogwabagole, mtuhumiwa akiwa anaishi na mwanaye wa kike baada ya kutengana na mkewake, akifahamu kuwa ni kosa la jinai alifanya mapenzi na mwanaye wa kuzaa na kumpa ujauzito mara tatu hadi mwaka 2017.

Katika hukumu inayomhusu Mmari, ilitolewa jana na hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama, Jasmine Abdul akisema ushahidi uliotolewa wa watu wanne hauna shaka.

Mshtakiwa huyo mkazi wa kijijij cha Kilingi wilayani Siha anadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 2 ,2018. Mwendesha mashitaka wa Serikali David Chisimba alisema mshtakiwa alimnywesha mtoto wake sumu aina ya dipu kwa madai ya kushindwa kumlea kutokana na maisha kuwa magumu, baada ya mwanaume aliyempa ujauzito kukimbia kusikojulikana.

Advertisement