Asilimia 20 ya ruzuku ya fidia haikupelekwa vijijini

Muktasari:

  • CAG amebaini jumla ya Sh3.32 bilioni zilizopokelewa kutoka Serikali Kuu kama fidia ya mapato ya halmashauri 62 hazikupelekwa kwenye Serikali za vijiji na kata.

Dar es Salaam. Kiasi cha Sh3.32 bilioni ambazo ni ruzuku ya fidia kutoka Serikali Kuu haikupelekwa vijijini, Mdhibiti wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebainisha hilo.

CAG amefafanua kuhusu fedha hiyo kuwa inatokana na hatua ya Serikali ya mwaka 2004 ya kufuta baadhi ya vyanzo vya ndani vilivyokuwa vinakusanywa na halmashauri za wilaya.

Kutokana na hilo Serikali Kuu hutoa ruzuku ya fidia ya vyanzo vilivyofutwa, ambapo mamlaka za Serikali za mitaa ziliagizwa kupeleka asilimia 20 ya kiasi kilichopokelewa katika ngazi ya kata na vijiji.

“Katika ukaguzi huu, nimebaini kuwa jumla ya Sh3.32 bilioni zilizopokelewa kutoka Serikali Kuu kama fidia ya mapato ya halmashauri 62 hazikupelekwa kwenye Serikali za vijiji na kata,” alibainisha CAG kwenye ripoti yake ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2017/18 iliyowasilishwa bungeni Aprili 10, 2019.

CAG alipendekeza kuwa mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa asilimia 20 ya fidia ya vyanzo vya ndani inayopokelewa kutoka Serikali Kuu inapelekwa kwa wakati kwenye serikali za vijiji na kata ili zikatekeleze shughuli mbalimbali walizojipangia.