Asimulia miaka 18 ya ndoa yake na anayedaiwa kumchemsha mwanae

Wednesday June 26 2019

 

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected]

Tukio la mwanamke Happyness shadrack (35) kudaiwa kumkatakata mwanae wa kumzaa mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu kisha kuchemsha mabaki ya mwili wake jikoni limeshangaza jamii na kuwaacha wengi midomo wazi huku kila mmoja akisema lake.

Licha ya kuandika habari, lakini naguswa kufika katika familia ya mwanamke huyo kujua maisha ya Happynes yalikuaje kabla ya tukio hilo.

Mapema asubuhi naanza safari ya kwenda Kijiji cha Buligi, Kata ya Senga wilayani Geita, ni kama kilomita 72 kutoka mjini Geita.

Nikiwa kituo cha mabasi mjini Geita habari inayojadiliwa ni madai ya mama kuua mwanae na kumchemsha.

Njia nzima jambo linalojadiliwa ni je, kitendo kile ni ugonjwa wa kawaida au ni ‘ndagu’ kwa watu wa kanda ya ziwa neno hili linamaanisha kitu anachofanyiwa au kukifanya mtu kwa lengo la kupata au kumpatia mtu utajiri.

Simulizi ya Mume wa Happynes

Advertisement

Safari yangu inanifikisha kijijini Mwatulole, napokelewa na watoto ambao wananipeleka kwa Yakobo Mtani baba wa watoto sita, sasa wakiwa wamesalia watano, namkuta akiwa amekaa pembezoni mwa nyumba huku uso wake ukionyesha ni mwenye majonzi.

Baada ya salamu na utambulisho, Mtani anaanza kunisimulia maisha yake na mkewe aliyeishi naye katika ndoa kwa miaka 18 sasa.

Mtani anasema Juni 3, 2019 akiwa kwenye biashara zake (kuuza viatu) alipigiwa simu na mkewe akimtaka arudi nyumbani. Anasema sio kawaida yake kurudi nyumbani siku za katikati ya wiki na kwamba yeye hurudi siku za mwisho wa wiki, lakini aliitikia mwito na kurudi.

“Nilikua Nyarugusu, kutokana na wito nilirudi nyumbani. Nikiwa njiani alipiga tena simu akaniambia si umesema unakuja mbona hufiki nikamwambia nakuja. Nilipofika nyumbani mke wangu alianza kuniomba msamaha akisema nisamehe mume wangu tutubu hii familia nzima itakufa”.

Anasema kauli ile ilimshangaza kwa kuwa sio kawaida ya mkewe kuwa kwenye hali hiyo “nilimuuliza kuna nini, lakini alikazana kusema nisamehe mume wangu tutubu maana sote tutakufa” anasema.

Mtani anasema kwa kuwa ilikua usiku wa saa nne, alimtuliza mkewe na kulala hadi asubuhi alipompeleka kwenye vipimo na kuelezwa mkewe ana malaria kali na kulazwa.

Anasema hospitali alikaa kwa siku tano akitibiwa malaria, typhod na UTI na baadae aliruhusiwa kurudi nyumbani, lakini mwili wake ulikuwa umechoka.

Mtani anasema wakati akiwa hospitali mama mzazi wa mkewe alifika kumuuguza. Baada ya kuruhusiwa alirudi na mkewe nyumbani, baadae walipigiwa simu kuwa mdogo wa mkewe alikuwa naumwa.

Kwa mujibu wa Mtani, kutokana na taarifa hiyo mama aliomba kuondoka na Happiness ili yeye (Mtani) aweze kuendelea na shughuli zake za kutafuta kipato na kulea watoto wengine jambo aliloliridhia.

Anasema mkewe na mama mkwe walianza safari na walikuwa wakiwasiliana kwa simu hadi Alhamisi, Juni 20, 2019 alipopigiwa simu na mama mkwe na kuelezwa kuwa mgonjwa anakosa usingizi, halali kabisa usiku. Hivyo Mtani akapanga kwenda kumchukua Jumamosi ili ampeleke tena hospitali.

“Kabla sijakwenda, Ijumaa nikiwa kibaruani ndipo nikapigiwa simu kuelezwa kuwa inadaiwa mke wangu kamuua mtoto wetu na kumpika..leo mwanangu kauawa kama mbwa mke wangu yupo mahabusu hata hanitambui,” anasimulia na kuinama huku machozi yakimtoka.

“Naumia sana ninapoenda kumuona mke wangu akiwa mahabusu wala hanitambui tena sijui kilichompata mke wangu lakini Mungu yupo na kama anasikia kuomba kwetu basi naamini ipo siku atajibu na kisasi cha Mungu kitakua kikali zaidi.“

Mtani anasema ameishi na mkewe kwa miaka 18 wakiwa na ndoa yenye amani, furaha licha ya kwamba wakati mwingine hutokea kupishana kauli lakini muda mwingi ulikua wa amani na furaha.

Ni mpambanaji katika maisha

Anasema mkewe ni mwanamke mpole, jasiri asiyechagua kazi na alikua akifanya ‘deiwaka’ (vibarua). Yeye ukimpa kazi ya ujenzi anajenga, kulima atalima alikuwa akijishughulisha na kazi yoyote inayokuja mbele yake.

“Mke wangu ndiye aliyekuwa akilisha familia na fedha ninayopata tunakusanya tukanunua kiwanja na kuanza ujenzi wa hii nyumba unayoiona. Kabla haijakamilika akahimiza tuingie hivi hivi tuache kulipa kodi, tusomeshe watoto sijui nisemeje kuhusu mke wangu kama kweli Mungu yupo basi kwenye hili adhihirike na naamini hataacha lipite hivi,“ anasema Mtani.

Mtani anasema kwa miaka 18 aliyoishi na mkewe hajawahi kuugua na kulazwa tofauti na kipindi hiki, na kuiomba Serikali kutoa nafasi ili atibiwe kabla tatizo halijakomaa.

Mama aeleza alivyoishi na watoto wawili wenye tatizo la akili

Lucy Shadrack mkazi wa kijiji cha Buligi kata ya Senga ni mama wa watoto wanane Happiness akiwa mwanae wa pili kuzaliwa. Anasema kilichotokea kwenye familia yake ni kigumu na hakielezeki “kuwa na watoto wawili wagonjwa kwa wakati mmoja, ugonjwa uleule sio jambo dogo naumia.”

Mama huyo anasema wanae hao ambao ni wa pili kuzaliwa na wapili kutoka mwisho wameugua kwa mwezi mmoja sasa.

Akielezea kuugua kwa watoto wake anasema amewahi kulazwa hospitali ya Upendo iliyopo mjini Geita baada ya kuelezwa kuwa na malaria kali na baada ya kumaliza sindano za Quinini aliruhusiwa kurudi nyumbani.

Anasema baada ya kurudi naye kijijini hapo Juni 21, 2019 asubuhi alilazimika kwenda kutafuta dawa za usingizi na kumuacha mwanae akiwa na mjukuu aliyekuwa akimsaidia mtoto “sikuwa na hofu kwa kuwa huwa nawaacha na nikirudi nawakuta wakiwa salama.”

“Niliporudi nilikuta amebandika sufuria jikoni anachochea moto nilimuuliza unapika nini akasema anachemsha maji nikamuuliza mbona maji yapo ndani akadai anachemsha mbuzi aliyopewa na mchungaji kufunua sufuria ndipo nikakuta vipande...nilishtuka sana,” anasema.

“Niliingia ndani ndipo nikakuta damu chumbani na kisu kidogo. Nilimuita mjukuu niliyemwachia mtoto ili nijue mtoto aliko akadai alilala, akamlaza kitandani…nilikimbia hapa kwa jirani ambae ni mchungaji tukaja nae hapa akatoa sufuria jikoni ukimuuliza Happiness amefanya nini yeye anasema anapika mbuzi,” anasema.

Mchungaji Amoni Mtani wa Kanisa la Faith Mission na jirani alifika nytumbani hapo anasema tukio hilo ni la kushangaza na mazingira yake bado yanawaacha watu vinywa wazi wasijue la kusema.

Hata hivyo, anasema anaviamini vyombo vyenye mamlaka kwamba vitatenda haki kuchunguza na kubaini undani wa tukio hilo.

Advertisement