Askari polisi akutwa amekufa baa

Muktasari:

Tukio hilo limetokea Machi 13 saa 4:30 usiku baada ya askari Polisi Donald Motoulaya kufika katika Baa ya Friends na kwenda kulala kwenye makochi yaliyowekwa katika moja ya vyumba vya baa hiyo bila wahusika kujua.

 

Songea.  Askari Polisi, PC Donald Motoulaya (29) wa ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, amekutwa amefariki dunia akiwa kwenye baa iitwayo Friends Pub iliyopo Manispaa ya Songea mkoani humo.

Akizungumza  na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoani  Ruvuma, ACP Simon Marwa alisema tukio hilo limetokea Machi 13 saa 4:30 usiku.

Kamanda Marwa alisema Motoulaya kabla ya kifo alianguka kwenye ngazi za mlango wa baa hiyo baada ya kujikwaa.

Kamanda huyo alisema mhudumu aliyejulikana kwa jina la Jaibu Nyoni (26), alimtoa nje na alifika kwenye baa hiyo akitokea baa ya karibu aliyoitaja kwa jina la Yapenda au Mtini Pub kwa lengo kujipatia kinywaji zaidi.

 “Baada ya kutolewa nje huku mhudumu akiendelea na shughuli zake, askari huyo  alijipenyeza na kuingia kwenye chumba cha ndani cha baa hiyo na kwenda kukaa eneo lililowekwa makochi. Huyu askari alikuwa ameyazoea mazingira ya baa hiyo, hivyo alikaa huko bila wahudumu kufahamu kama yupo,” alisema kamanda huyo.

Walibaini kuwa kuna mtu ndani kwenye kochi na amelala asubuhi walipokuwa wanafanya usafi.

Kamanda Marwa alisema wahudumu hao waliingiwa na hofu baada ya kumuita lakini hakuitika wala kuamka, ndipo wakaamua kutoa taarifa kituo kikuu cha polisi cha mjini Songea.

Alisema polisi walipofika walibaini kuwa askari huyo alikuwa amefariki dunia na kuuchukua mwili wake kwenda kuuhifadhi Hospitali ya Songea (Homso).