Askofu: Wekeni akiba ya chakula, kateni bima za afya

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha,Mhashamu Isaac Amani akitoa salamu za Ijumaa Kuu wakati wa ibada ya Umoja wa makanisa ya kikristo iliyofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha leo.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Isack Amani amewataka wananchi kuweka akiba ya chakula ili kujihami katika kipindi kigumu kijacho baada ya mvua kutonyesha kwa wakati.

Arusha. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Isack Amani amewataka wananchi kuweka akiba ya chakula ili kujihami katika kipindi kigumu kijacho baada ya mvua kutonyesha kwa wakati.

Akitoa salamu za Ijumaa Kuu leo Aprili 19, 2019 katika ibada ya umoja wa makanisa ya Kikristo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha amesema ipo hatari ya njaa hivyo kuwataka wananchi kuhifadhi chakula walicho nacho.

“Kuna hatari ya njaa, nitoe wito mhifadhi chakula mlichonacho na hamna tafuteni kwa njia halali ni lazima tuwe na utaratibu wa kuwa na chakula kwa siku zijazo mwenye kusikia asikie na msipochukua hatua utasali na Mungu atakuangalia,” amesema Askofu Amani.

Amesema uharibifu wa mazingira hasa kukata miti kwa ajili ya nishati ya mkaa, kuni, mbao pamoja na kufungua mashamba mapya kumechangia kwa kiwango kikubwa mvua kutonyesha kwa wakati na kusababisha upungufu wa chakula.

Ametoa wito kwa wananchi wote kupanda miti sehemu mbalimbali ili kurejesha hali ya uoto wa asili ulivyokua awali ili kuweka mazingira ya kuvutia mvua kunyesha.

Katika hatua nyingine, Askofu Amani ameonyesha mzigo mkubwa walionao wananchi katika kugharamia matibabu na kuwashauri wawe na bima ya afya ambayo itawapunguzia mzigo wa matibabu.

“Siku hizi kuna vilio kwenye familia mbalimbali, watu wanaugua wanaambiwa watoe fedha kwa ajili ya vipimo lakini hawana hizo fedha, wanaandikiwa dawa pia hawana hizo fedha mwisho ni kifo, hivyo bima ya afya ni lazima  kama unapenda maisha yako,” amesema Askofu Amani.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Solomon Masangwa katika kukumbuka siku ya Ijumaa Kuu amewaasa Wakristo kuwa nuru kwa ulimwengu na kuwa mfano katika maisha ya kumcha Mungu.

Amesema usiwe ni utaratibu wa kila mwaka kuhudhuria ibada ya Ijumaa Kuu bali waishi yale ambayo Bwana Yesu Kristo alikuja kuyakamilisha katika maisha ya mwanadamu kuishi maisha matakatifu.