Askofu Bagonza: Kuweni makini na wanaokuja kwa sura ya kutetea wanyonge

Muktasari:

Waumini na wananchi wametakiwa kuwa makini na wanaojifanya wanatetea wanyonge kumbe wanataka kazi ya kufanya kwa kutumia unyonge wao.

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Dk Benson Bagonza amewataka waumini na wananchi kuwa makini na wanaojifanya wanatetea wanyonge kumbe wanataka kazi ya kufanya.

Dk Bagonza ameyasema hayo leo Aprili 19, 2019 kwenye Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la KKKT Dayosisi ya Karagwe Usharika wa Kanisa Kuu Lukajange.

Amesema kuna kilio cha rushwa, ufisadi, ujinga na ubadhirifu wa mali ya umma lazima wapatikane watu walio tayari kuteseka kwa ajili ya kukomesha madhambi hayo.

“Kwa hili napenda niweke angalizo unyonge, maradhi, umasikini wetu si mtaji kwa wasaka tonge, bwana Yesu hakunufaika na mateso yale aliyoyapata msalabani,” amesema Askofu Bagonza.

“Tulionufaika ni sisi tuliokombolewa, wanaojitoa kutetea wanyonge wawe makini kutotumia unyonge wetu kujinufaisha kiuchumi, kisiasa na hata kiimani, hata kwenye imani tumevamiwa wapo watu wanajinufaisha, ” amesema.

Amesema “Wapo watu wanajifanya kutetea wanyonge ukiangalia kwa makini ana jambo lake, anajifanya kama anatetea kumbe anataka tuendelee kuwa wanyonge apate kazi ya kufanya.”

Kiongozi huyo wa kiroho amesema, “Lazima wawepo watu watakaojitoa kwa ajili ya wengine, watukanwe,  waitwe  majina mabaya waandikwe vibaya magazetini na mitandaoni, lakini naamini Mungu hawezi kuwaacha.”

Amefafanua  kuna maneno matatu yanasisitiza upendo wa Mungu kwa wanadamu ambayo ni kwamba jua liwake, mvua inyeshe Mungu yupo nao.

Amesema Mungu aliwapenda wanadamu kuliko hata mwanaye, upendo wa ajabu wa kutoa siyo kupokea, “Tumezoea kupokea kama ishara ya upendo.”

Amesema kwa misumari tu Yesu Kristo angedondoka kwa maumivu pale msalabani, lakini upendo ndiyo ulimuweka.

“Dhambi tuliyotenda ilileta uhasama kati ya mwanadamu na Mungu ili kurejesha uhusiano huo hatua mbalimbali zilifanyika zikashindwa kurejesha, hivyo mateso ya Yesu ilikuwa kafara ya kukomesha hiyo dhambi,” amesema Askofu Bagonza.

Amesema badala ya wenye vipara, wenye dhambi au pengine watu wafupi, kufa kama kafara, Yesu alikufa.

Amefafanua hakuna lolote mwanadamu amechangia katika kuupata wokovu, kazi yote inafanywa na Mungu mwenyewe aliyeshuka kumtafuta mwenye dhambi.