Askofu Bagonza: Vita ya rushwa inahitaji makomandoo saba

Pichani Askofu Dk Benson Bagonza akizungumza katika Kongamano la vijana la matumizi chanya ya mitandao jijini Arusha. Picha Mussa Juma

Muktasari:

  • Mbali ya Askofu Bagonza, Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume alipongeza uamuzi wa Mahakama Kuu kuwaengua wakurugenzi wa halmashauri kusimamia chaguzi mbalimbali nchini.

Arusha. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Dk Benson Bagonza amesema vita dhidi ya ufisadi, rushwa na wizi wa rasilimali za Taifa haiwezi kufanikiwa bila kushirikisha kile alichokiita makomandoo saba wazoefu.

Alisema hayo wakati akizungumza katika kongamano la vijana lililoandaliwa na taasisi ya Change Tanzania lililofanyika jijini Arusha jana.

Alitaja makomandoo hao kuwa ni; mitandao ya kijamii, vyombo huru vya habari, asasi za kiraia na taasisi zisizo za serikali, vyama vya wafanyakazi, vyama vya upinzani, Bunge huru na katiba nzuri.

“Kuwapunguzia uhuru makomandoo hawa au kugombana nao ni kutangaza kushindwa kabla ya mapambano kuanza,” alisema Askofu Bagonza.

Alibainisha kuwa matumizi chanya ya mitandao ya kijamii ni nyenzo nzuri ya utetezi katika jamii lakini wasioliona hilo ni wale wanaodhani kwa nafasi zao, hawahitaji kutetewa.

Alichambua mambo hayo saba na kubainisha jinsi yanavyoweza kutumika katika mapambano ya rushwa na ufisadi na hatimaye Taifa liondokane katika dimbwi rushwa na ufisadi.

“Mitandao ya kijamii ina nguvu ya udhibiti wa matumizi mabaya ya madaraka na dhambi nyingine katika jamii.

“Taifa letu chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, limetangaza vita kali dhidi ya ufisadi, rushwa na wizi wa rasilimali za Taifa. Ili kushinda vita hii, Serikali inahitaji msaada wa makomandoo wazoefu katika vita ya namna hii,” alisema.

Mbali ya Askofu Bagonza, Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume alipongeza uamuzi wa Mahakama Kuu kuwaengua wakurugenzi wa halmashauri kusimamia chaguzi mbalimbali nchini.

Fatma aliyekuwa akizungumzia hukumu ya kesi iliyofunguliwa na Bob Wangwe kupinga halmashauri za majiji, miji/wilaya na manispaa kusimamia chaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ina maana kubwa katika demokrasia ya Tanzania.

Alisema ili kujua tatizo la wakurugenzi kusimamia uchaguzi ni vyema kutambua aliyewateua na sheria ya uchaguzi inasemaje.

“Kuna sheria ya Serikali za Mitaa ambayo inazungumzia Rais kuteua wakurugenzi lakini kuna sheria ya uchaguzi ambayo inatambua hao wakurugenzi na kuwatumia.

“Watu wanapenda kulalamika lakini hawachukui hatua, tuige mfano wa Wangwe kwa kujitoa mhanga kufungua kesi hii,” alisema Fatma.

Kuhusu nia ya Serikali kukata rufaa, Fatma alisema hana pingamizi kwani watakutana mahakamani.

Hukumu hiyo ilitolewa Mei 10, 2019 na kuwaengua wakurugenzi hao kusimamia uchaguzi. Hata hivyo, Serikali imetangaza nia ya kukata rufaa kuhusu hukumu hiyo.

Mkurugenzi wa taasisi ya Change Tanzania Forum, Maria Sarungi alisema licha ya uwepo wa sheria kandamizi dhidi ya uhuru wa kujieleza katika mitandao, bado mitandao ya kijamii haikwepeki.

“Change Tanzania tutaendelea kusaidia uwepo wa uhuru wa kujieleza lakini tunataka badala ya kuwachukulia hatua, watumiaji wa mitandao wanapaswa kuelimishwa,” alisema Maria.