Awamu ya pili ya ETS yageukia vinywaji baridi, kuanza Agosti Mosi

Muktasari:

Mfumo huo unaelezwa kurahisisha na kuondoa usumbufu kati ya TRA na wazalishaji bidhaa

Dar es Salaam. Kuanzia Agosti mosi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), itaanza kutumia mfumo wa stempu za kielektroniki (ETS) katika bidhaa za vinywaji baridi kama soda na vinginevyo visivyo na kilevi.

Hata hivyo, vinywaji ambavyo vimeshaingizwa sokoni vitauzwa kama kawaida hadi Januari 31 mwakani.

Hii ni awamu ya pili ya kutumika kwa mfumo huu unaosimamiwa na kampuni ya Uswis iitwayo Societe Indusrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (SICPA).

Awamu ya kwanza iliyoanza Januari 15, ilikuwa ni kwa vinywaji aina ya bia, mvinyo na pombe kali.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, D Edwin Mhede Julai 24 ilieleza kuwa bidhaa mpya zote zilizotajwa awamu ya pili zinazozalishwa nchini na zinazoagizwa kutoka nje mpaka Januari 31 zinatakiwa kuwa na stempu hiyo.

Taarifa hiyo inasema TRA hivi karibuni itatangaza tarehe rasmi kwa ajili ya bidhaa nyingine ambazo hazijatajwa kwenye orodha ya awamu ya pili, ambazo ni juisi za matunda na mboga, maji na bidhaa za muziki na filamu.

Katika taarifa hiyo, Mhende aliwashukuru walipa kodi wote kwa ushirikiano wao kwa TRA ambao wamekuwa wakiuonyesha kufanikisha utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ETS.

Juni, mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo aliliambia Mwananchi kuwa takwimu zinaonyesha kuna ongezeko la ukusanyaji mapato kutokana na awamu ya kwanza ya mfumo huo. “Tuna imani mfumo huu utaongeza mapato, kwa awamu ya kwanza tu tumefanikia kuongeza mapato ya ushuru wa forodha kutoka Sh24 bilioni Januari hadi Sh28 bilioni Aprili,” alisema mpaka wakati huo mashine 44 za ETS zilikuwa zimefungwa katika viwanda mbalimbali nchini.

“Mfumo huu unarahisisha upatikanaji hesabu halisi za uzalishaji na malipo ya ushuru wa forodha bila kuingiliwa na mtu, tuliwiwa kufanya kazi na SICPA baada ya kuona mafanikio ya mfumo huu katika nchi za Kenya, Morocco, Uganda, Malaysia, Brazil, Turkey na Albania,” alisema Kayombo.