Aweso achongea wakandarasi wa maji ataka wasweke mahabusu

Muktasari:

Naibu Waziri wa Maji, Juma Aweso ameutaka uongozi wa mkoa wa Geita kuwashughulikiwa watekelezaji wa miradi ya maji katika wilaya ya Nyang’hwale, ameagiza wawili wakamatwe na mmoja kuwekwa mahabusu kwa kushindwa kukamilisha kazi zao kwa wakati.

Nyang’hwale. Naibu waziri wa maji Juma Aweso ameagiza kuwekwa ndani kwa Mkandarasi anayejenga mradi wa maji wa Nyamtukuza, Mwaipopo Lukas kutokana na kushindwa kuonyesha nyaraka za pampu ya maji aliyoiagiza nchi za nje miaka mitano iliyopita ambayo mpaka sasa haijafika.

Pia ameutaka uongozi wa Mkoa wa Geita kutumia mamlaka waliyonayo kumkamata Mkurugenzi wa kampuni ya PET Co-operation Limited pamoja na Mkurugenzi wa FAMOYO Ltd ambao kampuni zao zimeshindwa kukamilisha kwa wakati kazi tofauti za maji na kusababisha wananchi waendelee kuteseka.

Aweso amechukua uamuzi huo leo Mei 19 mwaka 2019, baada ya kutembelea mradi huo unaojengwa toka mwaka 2014 kwa gharama ya Sh15 bilioni na kukutana na wananchi waliomueleza namna wanavyoishi kwa kutumia maji ya mabwawa ambayo hata mifugo inanywea hapo.

Aweso amesema moja ya sababu iliyosababisha kutokamilika kwa mradi huo ni pamoja na kazi kutolewa kwa wakandarasi 11 ambao wanakwamishana kiutendaji na kuwataka wahandisi wa maji kufanya kazi kwa kufuata taaluma, weledi na kuacha kutoa kazi kwa wakandarasi kwa kujuana.

“Haiwezekani mradi Serikali imeshatoa bilioni tano lakini hakuna kijiji hata kimoja kilichopata maji na kila kiongozi anayefika mnadai mmeagiza pampu, kama wamekula hela watazitapika, ” amesema Aweso.

Awali mbunge wa jimbo la Nyangwale Hussein Kasu amesema mradi huo umekuwa ukitolewa maagizo na viongozi mbalimbali na wakiondoka hakuna utekelezaji  hivyo akamuomba Waziri kufanya maamuzi magumu kwakuwa wanaoteseka ni wananchi.