BAJETI: Wizara ya Viwanda ina vipaumbele 10 - VIDEO

Wednesday May 15 2019

By Ibrahim Yamola, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amewasilisha bajeti ya Sh100.38 bilioni kwa ajili ya mwaka 2019/20 ambayo ni pungufu kwa Sh43 bilioni, ikilinganishwa na ya mwaka 2018/19 na kutoa onyo kali kwa wafanyabiashara waliobinafsishiwa viwanda.

Katika bajeti hiyo iliyopungua kutoka Sh143 bilioni ya mwaka huu wa fedha, Waziri Kakunda alisema mwaka 2019/20 wizara itatekeleza vipaumbele 10.

Hata hivyo, bajeti ya mwaka jana ilikuwa pia ikishughulikia uwekezaji kabla ya Rais John Magufuli kuhamisha majukumu hayo katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Waziri alisema katika kiasi hicho kinachopendekezwa, Sh48.88 bilioni ni za matumizi ya kawaida na Sh51.5 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Ndani ya mwaka ujao wa fedha, wizara inatarajia kukusanya maduhuli ya Sh14.3 bilioni.

Alipokuwa akiomba kukusanya na kutumia Sh143 bilioni mwaka jana, aliyekuwa waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji, Charles Mwijage alitenga Sh100.02 bilioni kwa ajili ya maendeleo na zilizobaki kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Mwijage alisema Sh97.5 bilioni zingekusanywa kutoka vyanzo vya ndani na Sh2.5 bilioni zingetolewa na wahisani.

Akielezea utekelezaji wa bajeti iliyopo, Kakunda alisema hadi Aprili, wizara ilikuwa imepokea Sh43 bilioni, kati yake Sh30.85 bilioni ni za matumizi ya kawaida na Sh12.5 sawa na asilimia 12.4 za maendeleo.

Mwaka 2019/20, alisema wizara itaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara ikiwamo kuongeza ubora wa bidhaa na huduma. Vilevile, alisema itahamasisha wajasiriamali kuchangamkia masoko ya ndani na nje ya nchi.

Waliobinafsishiwa viwanda

Kuhusu tathmini ya viwanda 156, Waziri huyo alisema ni 88 pekee vilivyobinafsishwa vinafanya kazi na 68 vilivyobaki havifanyi kazi.

Kati ya viwanda 88 vinavyofanya kazi, alifafanua kuwa 42 vinafanya vizuri sana na 46 vinafanya kiasi cha kuridhisha.

Viwanda 20 alisema vimefutwa kwa sababu ubinafsishaji wake ulifanywa kwa kuuza mali moja moja na vingine kuruhusiwa kubadili matumizi.

Viwanda vingine 48 wamiliki wake wameshindwa kuviendesha na tayari 16 vimerejeshwa serikalini wakati wamiliki wengine 32 wakipewa notisi ya kuwasilisha mpango wa kuviendeleza kabla ya Mei 31.

Ukipita muda huo bila taarifa yoyote, Kakunda alisema viwanda husika vitarejeshwa serikalini ili vitatafutiwa wawekezaji wengine.

“Baadhi ya vilivyorejeshwa serikalini vimebainika nyaraka zake zilitumika kuchukulia mikopo mikubwa tofauti na thamani iliyotumika wakati wa ubinafsishaji na wakopaji wengine hawajalipa mikopo hiyo. Baadhi yao wameshindwa kukabidhi nyaraka za viwanda walivyokabidhiwa,” alisema.

Aliwatahadharisha wahusika popote walipo kwamba kutotoa nyaraka hizo ni kuhujumu uchumi wa nchi.

“Wahakikishe wamemalizana na benki kwa kulipa mikopo yao ifikapo Mei 31, 2019 na Serikali haitaongeza muda wa kuleta maelezo yanayoeleweka kuhusu viwanda hivyo, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaokaidi,” alisema.

Advertisement