UCHOKOZI WA EDO: Baada ya pingu za profesa zitakuja za wengine na wengine

Jinsi maisha yanavyokwenda kasi. Mtu ambaye uchaguzi mkuu uliopita alitembeza bakora kwa mwanachama mwenzake chamani, akaachwa huru bila kutiwa pingu na kushtakiwa kwa shambulio la aibu hadharani, leo ameamuru mtalaamu wa hisabati apelekwe kwake, ikiwezekana akiwa ametiwa pingu kwa kuongea kitalaamu katika eneo lake.

Wazungu wanasema mtu huyo hana moral authority. Yaani hata katika nafasi aliyopo hapaswi kuwepo. Yote yamesahaulika lakini juzi Taifa lilikuwa likimsikiliza bosi wa kile chombo akifoka na kutaka kiranja wa hesabu za Serikali aitwe Dodoma.

Kisa? Akiwa katika ardhi ya Donald Trump kiranja huyo amedai kwamba ule mhimili wa Dodoma haufanyi kazi yake vema pindi akiwasilisha hesabu zake.

Mimi ni darasa la saba. Sina uwezo mkubwa wa kujikita katika uhalali wa yule bosi wa Dodoma kumwita kiranja huyu katika himaya yake. Tayari kuna watu wametoa ufafanuzi wa kisheria. Mimi najikita katika maswali. Ni kweli mhimili huu wa Dodoma unaishughulikia Serikali hii vema?

Ni kweli huyu kiranja hajui anachokisema? Wote tunamjua jinsi alivyo makini, mcha Mungu na mtaalamu wa kazi yake. Anajua anachokisema. Nilidhani bosi wa mhimili wa Dodoma angetafakari kwa makini.

Nadhani hataki aguswe wala mhimili mkuu uguswe. Lakini tangu lini ufisadi uliondoka nchini? Bado upo na kauli ya kiranja ingechukuliwa kama changamoto badala ya kuanza kumtisha.

Sioni kama kuna kiranja yeyote anaweza kuchaguliwa pale akaja na ripoti safi ya matumizi.

Hisia zangu zinanituma kwamba kitu kingine ambacho kimewakera mabosi ni ardhi ambayo profesa kiranja ameitumia kutoa kauli hiyo.

Ni kwa Wazungu, Marekani. Imeonekana kama vile amekwenda kuchonganisha mambo hata kama aliongea kwa Kiswahili. Uhusiano wetu na Wazungu siku hizi si mzuri sana.

Mwishowe bosi wa mhimili ule wa Dodoma inabidi ajitafakari. Nani ana habari na chombo chake siku hizi? Hakina mvuto, kipo kimya. Baada ya profesa kwenda na pingu Dodoma nadhani watafuata wengine na wengine. Sidhani kama kuna ambaye ataamka na kusifia mhimili wa Dodoma.