Baba Beyonce aleta bangi Kenya

Wednesday August 14 2019

 

By Thomas Matiko

BABA’KE nyota wa muziki kutoka Marekani Beyonce Knowles, yupo mbioni kuleta biashara ya bangi nchini Kenya licha ya kuwa marufuku nchini.

Matumizi au biashara ya bangi nchini ni kinyume cha sheria ingawaje siku za hivi karibuni kumekuwepo na kampeni za kuitaka ihalalishwe. Na huku kukiwepo na kampeni hizo, kampuni ya baba’ke Beyonce mzee Mathew Knowles ifahamikayo kama Bangi Inc, imetuma ombi ya kutaka kuorodheshwa kwenye soko la hisa la Nairobi - Nairobi Securities Exchange (NSE).

Mzee Knowles ni mwanachama wa bodi ya Bangi Inc. Bodi hiyo ilimteua kuwa afisa mkuu wa mauzo na ndio sababu amekuwa akijitahidi kusaka masoko kote duniani huku jicho lake likiwa limetua kwenye soko la hisa la Nairobi.

Kulingana na taarifa yake Agosti 7 walituma ombi lao la kutaka kibali cha kuorodheshwa kwenye NSE na sasa wanachosubiri ni majibu baada ya utathmini.

“Soko la hisa la Kenya limeimarika sana katika kipindi cha miaka michache iliyopita na limeonyesha uwezo wa kuimarika hata zaidi. Hii inatupa fursa nzuri ya kujitosa kwenye soko hili lenye uwezo wa kuzalisha mabilioni ya dola,” afisa mkuu mtendaji wa Bangi Inc alinukuliwa. Kama ikifanikiwa kuidhinishwa kwenye NSE wawekezaji watakubaliwa kununua hisa kwenye kampuni hiyo kupitia Mpesa na Airtel Money.

Advertisement