VIDEO: Baba aeleza walivyowasiliana kwa mara ya mwisho na mwanafunzi wa KIU aliyeuawa

Thursday June 20 2019

mwanafunzi wa KIU,Assembles of God (TAG) Salasala, mwanafunzi wa KIU aliyeuawa

 

By Autea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Saa 9:30 jioni nikiwa nakaribia kuiacha barabara kuu ya mtaa wa Salasala magengeni kuingia katika nyumba ya Simpolianus Mgaya nakutana na umati mkubwa wa watu.

Watu hao walikuwa wamesimama katika makundi wakijadili mambo mbalimbali ambayo si rahisi kuyajua, lakini kadri nilivyozidi kusogea katika nyumba hiyo ya baba mzazi wa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Kimataifa cha Kampala (Kiu), Anifa Mgaya (21), sauti za watu waliokuwa wakiimba zilizidi kusogea.

Naam, zilikuwa nyimbo za mapambio kusindikiza msiba mzito ulioikumba familia yake na ile ya wanachuo na jamii nzima ya Kiu.

Hata hivyo, nyuma ya ujasiri wa kuimba nyimbo za maombolezo, wanakwaya hao wa Kanisa la Tanzania Assembles of God (TAG) Salasala, kulikuwa na huzuni kubwa ya kumpoteza muumini mwenzao na walikuwa wakijitahidi kuwafariji wazazi na ndugu wa binti huyo aliyekuwa mwaka wa pili akisomea stashahada ya maabara.

Binti huyo alifariki dunia Jumapili ya Juni 16, 2019 saa 2:30 usiku karibu na geti la chuo alichokuwa akisoma, eneo la Gongolamboto, Dar es Salaam baada ya kushambuliwa kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Umati wa watu uliokuwapo msibani hapo pamoja na viongozi wakubwa wa Serikali akiwamo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni na makamanda wa polisi wa wilaya za jiji la Dar es Salaam haukuweza kumzuia baba mzazi wa binti huyo kuonyesha machungu yake na kumwaga machozi.

Advertisement

Kumbukumbu ya mwisho ya familia

“Alikuwa binti ambaye tayari tumeanza kupata matumaini kuwa tumemjengea misingi imara ya kujitegemea ili aweze kujisaidia na kusaidia wenzake katika siku za usoni, lakini amekatishwa uhai wake,” baba mkubwa wa Anifa, John Mgaya alizungumza huku machozi yakimlenga.

Anifa alikuwa mtoto wa tatu katika familia yenye watoto saba huku kati yao wa kiume akiwa ni mmoja tu.

“Wiki moja kabla alikuja nyumbani na kuomba tumalizie kumlipia ada ili aruhusiwe kufanya mtihani, Jumatano tulimtumia hiyo fedha ila kutokana na kuwa ‘busy’ alituomba fedha hiyo aitoe Jumapili (siku ambayo umauti ulimkuta).

“Sasa hatujui kama alikuwa tayari ameitoa Jumamosi ili akafanye malipo ya ada, ni binti mtulivu, mchamungu aliyependa kumsaidia mama yake katika kila jambo alipokuwa nyumbani na alipenda michezo,” anasema Mgaya.

Licha ya matarijio makubwa ya wazazi, walezi au wasamariawema wanapowapeleka watoto wao shuleni ili waweze kuwa msaada hapo baadaye, lakini baadhi ya matukio ya kihalifu yamekuwa yakisababisha huzuni kwa wengine.

“Matukio ya wizi wa mali za wanafunzi, kukabwa na kuibiwa tumekuwa tukiyapokea sana kama Serikali ya wanafunzi, lakini hili la Anifa limetufundisha kuyafanyia kazi yote yanayoripotiwa,” anasema Makamu wa Rais wa Serikali ya wanafunzi Kiu, Dismas Meya.

Anasema kufanya hivyo kutawawezesha kuendelea kupata taarifa mpya za matukio wanayokutana nayo wanafunzi ili yafanyiwe kazi na kuhakikisha usalama wao unazingatiwa hasa kwa wale wanaoishi nje ya chuo.

“Tumefanya ukaguzi katika maeneo ya hosteli za nje ili kuhakikisha kuwa wako salama kwa sababu matukio kama haya yanakatisha ndoto za wanafunzi ambao baadhi ni tegemeo kwa wazazi wao,” anasema Meya.

Uhusiano wa wanachuo, jamii

Matukio ya uhalifu kama lililomfika Anifa wengi wamezoea kusikia yakifanyika usiku mkubwa watu wakiwa wamelala, lakini kilichotokea kwa binti huyo kinawashtua watu na kuhisi huenda kuna hali ya kutokuwapo kwa maelewano mazuri kati ya wanafunzi wa chuo hicho na wananchi wanaokizunguuka.

Chuo cha Kiu kipo karibu na makazi ya watu tofauti na vyuo vingine vilivyojitenga kama ilivyo kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mzumbe au Sua vilivyoko Morogoro.

Ukitoka tu nje ya geti la Kiu kilichopo Gongolamboto, utapokelewa na msururu wa nyubumba za kuishi. Hatua chache kutoka lilipo geti la kuingilia chuoni hapo vijana wa bodaboda, wauza vyakula na watoa huduma zingine wanaendesha shughuli zao.

Wanafunzi wengi wa Kiu kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakipanga vyumba na kuishi katika mazingira yanayokizunguuka chuo hicho.

“Mahusiano kati yetu na wananchi wanaozunguuka chuo ni mazuri, ndiyo maana baadhi ya wanafunzi wanaweza kuishi katika nyumba zao na kuendelea na shughuli za kimasomo kama kawaida ila kilichowapata ni hofu ya kusema endapo wakisaidia polisi au kutoa maelezo wanaweza kuingia matatizoni ndicho wanachoogopa.”

“Jeshi la polisi inabidi liangalie suala hili mara mbili kwa sababu wakati mwingine wananchi wanakuwa na uwezo wa kusaidia watu wanaodhurika ila wanakuwa na hofu ya kuhusishwa katika tukio hilo.”

Kwa mujibu wa George Jackson ambaye ni mwenye nyumba aliyokuwa akiishi Anifa, katika muda wote wa masomo yake binti huyo alikuwa hana tabia ya kurudi nyumbani zaidi ya saa tatu usiku.

“Saa mbi huwa anakuwa ametoka kujisomea chuoni, akichelewa sana ni saa tatu anakuwa ndani, hana marafiki wa nje kwa kuwa marafiki zake wote walikuwa na vyumba kwenye nyumba yangu hivyo siyo rahisi wao kwenda kuongea nje ya nyumba.”

Kwa maelezo ya pande mbili hizo ni dhahiri ipo haja ya kuchimba na kufahamu kitu gani kinachochea kutokea tukio kama hilo hasa ikizingatiwa kuwa uhusiano ni mzuri. Huenda kuna vibaka wanaotumia mwanya wa mwingiliano wa wananchi na wanachuo kutekeleza uhalifu, juhudi zifanyike usalama uimarishwe na matukio ya uhalifu yanayodaiwa kutendeka mara kwa mara dhidi ya wanafunzi yakomeshwe.

Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assembles of God (TAG) John Siame anasema licha ya Anifa kuishi chuoni muda mwingi, lakini alikuwa na tabia ya kuulizia ratiba ya ibada kila anaporudi likizo ili aweze kuhudhuria.


Advertisement