Baba asimulia mwanawe alivyouawa akiimba nyimbo za utukufu

Muktasari:

Baba huyo amesema mwanawe alikuwa akiimba nyimbo za utukufu na ndiye aliyekuwa msaidizi wa mchungaji ambaye hakuwapo siku hiyo.


Dodoma. Mazishi ya Isaka Petro (28) anayesadikiwa kuuawa na mkurugenzi wa halmashauri ya Itigi yalifanyika jana nyumbani kwao Kijiji cha Kazikazi lakini waumini wamesimulia kuwa alikufa wakati akiimba.

Petro aliuawa kwa kupigwa risasi Jumamosi ya Februari 2,2019 na kuzikwa jana baada ya utata wa kifo chake ambapo mazishi yake yaliongozwa na Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jafo aliyetoa ubani wa Serikali wa Sh1 milioni.

Baba mzazi wa Isack, Petro Chambalo amesema uwanja wa kanisa siku hiyo uligeuka kuwa vita na milio ya bunduki na kwamba walijua dunia imekwisha.

"Lakini mwanangu alikufa akiimba nyimbo za utukufu, yeye hakujibu kitu zaidi ya kuamua wakati mkurugenzi na mtendaji wa kijiji walipokuwa wanamtoa muumini nje," amesema Petro.

Amesema siku hiyo marehemu alikuwa anaongoza ibada kwa kuwa alikuwa ni msaidizi wa mchungaji na katika ibada hiyo mchungaji hakuwepo.