Bajeti Wizara ya Fedha ni Sh 11.9 trilioni, vipaumbele 16

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Wizara ya Fedha na Mipango leo Jumatatu Juni 3, 2019 imewasilisha bajeti yake yam waka 2019/2020 ya Sh11.98trilioni. bajeti ya wizara hiyo mwaka 2018/19 ilikuwa Sh12.05trilioni.

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo mwaka 2019/2020 ya Sh11.94trilioni, kati ya fedha hizo Sh730 bilioni ni kwa ajili ya maendeleo.

Dk Mpango mbali na kufafanua matumizi ya kiasi hicho cha fedha, ameeleza vipaumbele 16 vya wizara hiyo mwaka 2019/2020.

Bajeti ya Wizara hiyo mwaka 2018/19 ni Sh12.05 trilioni na kati ya fedha hizo Sh10.76 trilioni zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh1.29 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Hadi Aprili, 2019 wizara hiyo ilikuwa imepokea Sh8.25 trilioni sawa na asilimia 68.46 ya bajeti iliyoidhinishwa.

Akizungumza bungeni leo Jumatatu Juni 3, 2019, Dk Mpango amesema kati ya Sh11.94 trilioni za bajeti ya 2019/2020, Sh11.2 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh730.58 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Dk Mpango amesema matumizi ya kawaida yanajumuisha Sh608.3 bilioni za mishahara na Sh10.60trilioni ya matumizi mengineyo.

“Matumizi ya maendeleo yanajumuisha Sh677 bilioni fedha za ndani na Sh53.58bilioni ni fedha za nje,” amesema Dk Mpango.

Kuhusu bajeti ya 2018/19, Dk Mpango amesema kati ya Sh8.25 trilioni zilizopokelewa hadi Aprili 2019, Sh8.23 trilioni  ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 76.49 ya bajeti iliyoidhinishwa na Sh20.68 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

“Kati ya fedha zote za maendeleo zilizopokelewa Sh15.37 bilioni ni fedha za ndani, na Sh5.31 ni fedha za nje,” amesema Dk Mpango.

Amesema hadi Aprili 2019, wizara imetumia Sh7.03 trilioni kwa ajili ya matumizi mengineyo pamoja na deni la Serikali, sawa na asilimia 67.30 ya fedha zilizoidhinishwa.

“Kati ya fedha hizo Sh301.61 bilioni zimetumika kwa ajili ya matumizi mengineyo, sawa na asilimia 67.72 ya fedha zilizoidhinishwa na Sh6.73 zimetumika kulipa deni la serikali na huduma nyingine sawa na asilimia 67.28 ya fedha zilizoidhinishwa,” amesema Dk Mpango.

 

Majukumu ya wizara 2019/2020

1.       Kubuni na kusimamia utekelezaji wa sera za uchumi jumla

2.       Uandaaji na ufuatiliaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa

3.       Kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani

4.       Kuratibu upatikanaji wa misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo

5.       Kubuni na kusimamia mifumo ya taarifa za fedha

6.       Usimamizi wa malipo

7.       Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa bajeti ya Serikali

8.       Usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma

9.       Usimamizi wa mali za Serikali

10.      Udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu na udhibiti wa ugaidi

11.      Tume ya pamoja ya fedha (vikwazo vya biashara)

12.      Usimamizi wa mashirika na taasisi za umma, uratibu wa mikakati ya kupunguza umasikini

13.      Ununuzi wa umma

14.      Ubia kati ya sekta binafsi na umma

15.      Mafao ya kustaafu na mirathi

16.      Michango ya mwajiri  kwenye mifuko ya hifadhi za jamii