Balozi Mwapachu amzungumzia Mengi katika maeneo saba

Muktasari:

Balozi Mwapachu aeleza uhusiano wake na Mengi na kuweka wazi mambo saba aliyoyafahamu kwake wakati wote wa urafiki wao

Dar es Salaam. Balozi Juma Mwapachu ameelezea uhusiano wake wa miaka 38 na aliyekuwa mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi huku akitaja mambo saba ambayo amekuwa akiyafahamu kwa rafiki yake huyo wa karibu.

Akizungumza leo Jumanne Mei 7, 2019 Balozi Mwapachu amemtaja Mengi kama tu  aliyekuwa na imani ya kina kwamba ndoto, fikra, uwezo na  mafanikio yake yalitokana na kuwezeshwa na Mungu, kumweka mbele kwa kila alilokuwa analifanya.

Mwapachu amesema Mengi aliukataa umaskini na alikuwa akisumbuliwa  na umaskini watu katika nchi yetu yenye utajiri mkubwa wa rasilimali.

“Kwake hali hii inasababishwa na sera bora na imara za uchumi na huduma za jamii hasa upande wa elimu na afya. Alishukuru sana Magufuli alipoingia madarakani kujaribu kubadili hali hii,” amesema Mwapachu.

Jambo lingine ambalo Mengi aliguswa nalo ni hali ya walemavu nchini na kukosekana mipango thabiti ya kubadilisha fikra za wananchi kuhusu walemavu.

Mwapachu amesema  maoni ya Mengi  yalikuwa ni kwamba wenye ulemavu hasa albino wana uwezo ambao unahitaji kuamshwa, kuhamasishwa na kuwezeshwa.

Jambo la nne  ni kwamba pamoja na kuonekana tajiri  Mwapachu amesema Mengi  hakuridhika na mafanikio aliyoyafikia alifurahishwa na mtazamo wa rais wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na ndiyo maana alianza kuanzisha viwanda mbalimbali.

Balozi Mwapachu amelitaja jambo la tano kuwa ni uwezo wa Mengi wa  kutambua nguvu kubwa ya vijana wanaomaliza shule na vyuo nchini ambao hawapati kazi, alianzisha mipango na taratibu za kuamsha ufahamisho wa fursa zilizopo na jinsi ya kupata mitaji.

Amesema Mengi hakujihusisha na siasa lakini sio kwamba hakuwa na mawazo ya kisiasa, muhimu kwake ilikuwa ni kujenga mazingira  na mahusiano mazuri kati ya Serikali na sekta binafsi.

Katika jambo la saba Balozi Mwapachu amemtaja Mengi kama  mwanamazingira, akieleza kuwa aliguswa na laana ya tabia nchi inayoathiri mazingira na vyanzo vya maji na alikuwa kinara wa kuhamasisha na kupanda miti kwenye misitu kuzunguka mlima Kilimanjaro.