Balozi wa Marekani nchini Tanzania aonywa

Thursday June 20 2019

Balozi  Marekani , Tanzania,Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki , Tanzania, Dk Faraji Mnyepe ,

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania  imeuonya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa kitendo cha kutoa taarifa za angalizo la kutokea kwa  shambulio la kigaidi na kuitaka kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia.

Onyo hilo la Tanzania limetolewa leo Alhamisi Juni 20, 2019 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia taarifa ya Ubalozi huo ilioutoa jana Jumanne.

Taarifa iliyowaingiza matatani ni ile iliyotolewa  jana jioni na ubalozi huo ikieleza kuwapo kwa uvumi wa kutokea kwa shambulio la kigaidi katika eneo la Masaki, Dar es Salaam nchini Tanzania hususan hoteli za kitalii na maduka ya maeneo hayo ya ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyotolea leo Alhamisi imesema ilimwita Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk Inmi Patterson ili kutoa ufafanuzi wa taarifa hiyo.

Hata hivyo, Ubalozi huo ulimtuma mwakilishi wa Dk Inmi ambaye ni Janine S. Young kwenda kuitikia wito huo wa Serikali ya Tanzania ambaye alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Dk Faraji Mnyepe. 

Katika taarifa hiyo imesema Janine S. Young amekiri kufanya makosa kwa kutoa taarifa  katika mitandao ya kijamii “Twitter” kuhusu angalizo la kiusalama.

Advertisement

“Amekiri kuwa ubalozi umefanya makosa ya kutoa tetesi ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee bali wote wakitambua kuwa ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania,” inasema taarifa hiyo.

 

“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeukumbusha Ubalozi wa Marekani umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani kote katika utoaji wa taarifa za aina hii,” ameongeza

Taarifa hiyo imemnukuu, Dk Mnyepe akiwataka wananchi na Jumuiya za Kimataifa pamoja na wageni mbalimbali waliopo nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwani.

Amesema mpaka sasa hakuna taarifa yeyote iliyothibitishwa ya kuwepo kwa tishio la aina hiyo hapa nchini na kwamba Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimejizatiti kukabiliana na matishio yeyote.

 


Advertisement