Balozi wa Uholanzi asema ni muhimu kuwekeza kwa wasichana

Wednesday June 19 2019

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Jeroen Verheul amesema uwekezaji kwa watoto wa kike ni muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa Taifa na uchumi jumuishi.

Balozi Verheul ameyasema hayo leo Jumatano Juni 19,2019 wakati akifungua warsha iliyoandaliwa na Muungano wa Mataifa katika Kuhifadhi Maliasili (IUCN) na kuwakutanisha wadau katika kujadili ukuaji wa uchumi jumuishi (Inclusive Green Growth).

Amesema Tanzania bado inakabiliwa na changamoto ya usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume huku wanawake wakiachwa mbali katika mambo muhimu kama vile elimu.

"Kuelimisha watoto na kudhibiti ongezeko la watu ni mazao ya ukuaji wa uchumi. Ni muhimu sana kuwekeza kwa wasichana ili kukuza uchumi wa nchi," amesema Balozi huyo na kuongeza kuwa kuna haja ya kupunguza pengo la kijinsia lililopo.

Verheul amesema ni wakati sasa kutafakari ni jinsi gani maliasili zinazopatikana hapa nchini zinachangia katika kuifanya Tanzania kufikia malengo yake ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kugusa maisha ya wananchi wote.

Advertisement