Bandari Dar yavuka malengo mapato, shehena

Thursday December 20 2018

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Ufanisi katika shehena kwenye Bandari ya Dar es Salaam umefanya iongeze mapato na kuvuka lengo la robo ya kwanza ya mwaka 2018 kutoka Sh202.2 bilioni hadi Sh206.5bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea ofisini kwake wiki hii, meneja wa bandari hiyo, Fredy Liundi alisema katika robo ya kwanza iliyoanzia Julai Mosi hadi Septemba, shehena ya mizigo isiyo kwenye makasha (general cargo) imefikia tani milioni 3.2 juu ya lengo la tani 2.9 ikiwa ni ongezeko la tani 244,272 sawa na asilimia tisa.

Kwa upande wa kontena alisema bandari hiyo imehudumia kontena 184,200 juu ya lengo la kontena 154,171 ikiwa ni ongezeko la kontena zaidi ya 26,000 sawa na ongezeko la asilimia 17 na juu ya kiasi kilichohudumiwa mwaka uliopita katika kipindi kama hicho ambapo jumla ya kontena 169,974 zilihudumiwa.

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho shehena ya mizigo ya kwenda nje inayopitia bandari hiyo imeongezeka ambapo imehudumia asilimia 81.2 ya mizigo inayopitia bahari kuu kwenda nchi za Zambia, DRC, Burundi, Rwanda Uganda na inayobaki nchini.

“Matokeo haya yanatokana na maboresho makubwa tuliyofanya katika bandari yetu ya kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi tukisaidiwa na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo sasa hivi mtu anaweza kuandaa ankara akiwa ofisini kwake popote pale na kufanya malipo kisha kuja kuchukua mzigo wake,” alisema.

Alisema kutokana na maboresho hayo wameweza kuvuka lengo la muda wa kuhudumia meli kutoka siku tatu na kufikia kuhudumia meli kwa siku 2.1 kwa upande wa kontena na siku 2.8 kwa meli za mizigo isiyokuwa kwenye kontena.

 


Advertisement