VIDEO: Bandari ya Bagamoyo ingefilisi, kuuza nchi

Muktasari:

Pamoja na kusamehewa kodi na ushuru mbalimbali kama zile za lazima kisheria, kulipwa fidia ya hasara ya kibiashara watakayopata kwa mujibu wa mahesabu yao, mwekezaji pia aliweka sharti la kuachiwa ajipangie bei ya kuwatoza watakaosafirisha mizigo kupitia bandari hiyo,.

Mwanza. Wakati Watanzania wa kawaida, wabunge na Spika Job Ndugai wakiendelea kujiuliza kwanini Serikali imesitisha majadiliano kuhusu uwekezaji kwenye mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, imebainika kuwa Serikali ingefilisika iwapo ingekubali masharti ya mwekezaji.

Pamoja na kusamehewa kodi na ushuru mbalimbali kama zile za lazima kisheria, kulipwa fidia ya hasara ya kibiashara watakayopata kwa mujibu wa mahesabu yao, mwekezaji pia aliweka sharti la kuachiwa ajipangie bei ya kuwatoza watakaosafirisha mizigo kupitia bandari hiyo,.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedith Kakoko akizungumza leo Jumapili Mei 19,2019 na Mwananchi katika mahojiano maalumu Jijini Mwanza, amesema licha ya Serikali kukubali kusamehe ushuru wa stempu, ukaguzi wa forodha (customs inspection) ile ya ukaguzi wa meli ambayo ni tozo ya Kimataifa na kufungua kituo (one stop center) cha kuhudumia biashara katika bandari ya Bagamoyo, mwekezaji aliibua masharti mengine mapya 14 yasiyotekelezeka.

 Kakoko ametaja masharti mapya yaliyoibuliwa na mwekezaji kuwa ni ya kusamehemewa kodi ya mapato, kodi ya taasisi, kodi ya ongezeko la thamani ya mali, kodi ya mapato kwa watu binafsi, ushuru wa Seriali za mitaa na kodi ya majengo.

“Mwekezaji pia alitoa mashari ya kusamehewa tozo ya ardhi, kodi ya fidia kwa wafanyakazi, kodi ya uendelezaji wa ujuzi, kodi ya forodha na kodi ya ongezeko la thamani, VAT.

“Walitaka wasamehewe kodi, ushuru na tozo zote za vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini; hii ingesababisha wageni, hata wasiohitajika wala kuwa na kazi ya kufanya kujazana nchini,” amesema Kakoko.

Amesema mwekezaji aliweka masharti hayo kwa kisingizio kwamba hakuna shehena ya kutosha na kuhoji inakuwaje mwenye fedha awekeze kwenye biashara isiyolipa.

“Hakuna shehena ya kutosha wakati wewe (mwekezaji) unataka kuwekeza kwenye reli na bandari. (Ni lazima) Unakuja kwa sababu biashara ipo” amesema Kakoko

Amesema masharti hayo yangekubaliwa, ni dhahiri Taifa lingeambulia sifuri huku mwekezaji akichukua asilimia 100 ya kila kinachopatikana licha ya ukweli kwamba pande zote zimewekeza.

Mkurugenzi Mkuu huyo ametaja ardhi, rasilimali watu na nguvu kazi pamoja na mazingira bora ya uwekezaji uliopi nchini kuwa ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali huku mwekezaji akitakiwa kuleta mtaji.

“Wakilegeza masharti na kukubali tugawane sawa sawa hakuna tatizo; waje na fedha zao. Lakini wahakikishe nasi tunapata. Haiwezekani sisi tupate sifuri lakini wao wapate asilimia 100,” amesema