VIDEO: Bandari ya Dar es Salaam kuanza kupokea meli inayobeba makontena 6,000

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kuboresha mazingira ya Bandari ya Dar es Salaam ili kuanza kupokea meli kubwa.

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwele amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam ili kuanza kupokea meli kubwa zinazobeba makontena mengi kati ya 4,000 mpaka 6,000.

Amesema meli zilizokuwa zinapokelewa awali ni zile zenye uwezo wa kubeba makontena 3,000 tu.

Akizungumza wakati wa ziara ya Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi alipoitembelea Bandari ya Dar es Salaam Kamwele amesema bandari ya Dar es Salaam ndiyo iliyo rahisi kutumiwa na wafanyabishara wa nchi jirani ikiwamo Congo.

Kamwele amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ikiwamo ujenzi wa magati.

  “Tunajenga vizuri kama unavyoona hiyo lami ni mpya na tumeongeza kina kwenda mita 15 ili ije meli yenye uwezo wa kubeba kontena  4,000 mpaka 6,000,” amesema Kamwele na kuongeza;

“Wizara yangu kila wakati inakaa vikao na wafanyabishara wa Congo na hapa tulipo kuna wananchi wengi wa Congo,” amesema Tshisekedi wa Congo.

Kabla ya kutembelea bandari hiyo Rais Tshisekedi alitembelea mradi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge  unaoendelea kujengwa nchini.

Reli hiyo inajengwa  kuanzia katika bandari ya Dar es Salaam inatarajia kufika katika nchi za Rwanda, Burundi na Congo.

Mwisho.