Baraza la Uongozi CUF kumjadili mrithi wa Maalim Seif

Muktasari:

  • Baraza Kuu la Uongozi CUF kukutana kesho kujadili nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho. Kwa sasa Katibu Mkuu ni Maalim Seif Sharif

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) kuitishwa kesho Jumamosi Machi 16, 2019 ili kujadili jina la mrithi wa nafasi ya Katibu Mkuu.

Hatua hiyo ya CUF imekuja baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa kanda ambao umefanyika kwa siku tatu juzi jioni, jana na leo Ijumaa ili kupata wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi.

Kwa mujibu wa mabadiliko ya katiba ya chama hicho, mwenyekiti atateua majina matatu kwa kushauriana na makamu wenyeviti wa chama hicho Bara na Zanzibar kisha majina yatawasilishwa kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi na kuchagua jina moja.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Machi 15, 2019 Mkurugenzi wa Habari wa CUF Abdul Kambaya amesema uchaguzi wa kanda umekamilika mapema asubuhi leo watajulikana wajumbe wa Baraza Kuu ambao watafanya mkutano wao wa kwanza kesho.

"Hivi tunavyozungumza nipo kwenye kikao, viongozi wakuu nao wana kikao kabla ya kuitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi hapo kesho kujadili majina yatakayowasilishwa na Mwenyekiti ili kumpata Katibu Mkuu wa chama," amesema Kambaya.

Kambaya amefafanua kuwa leo na kesho hakutakuwa na taarifa yoyote hadi vikao hivyo vimalizike.

"Kwa hali ilivyo na vikao vinavyoendelea tutatoa taarifa Jumapili, kuna uwezekano mkubwa siku hiyo Katibu Mkuu akawa ameshapatikana kama vikao vitakwenda kama ilivyopangwa," amesema Kambaya.