Baraza la madiwani Tanga lawafukuza watumishi 11

Thursday May 16 2019

By Burhani Yakub, Mwanamchi [email protected]

Tanga. Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga limewafukuza kazi watumishi wake 11 na mwingine kushushwa mshahara kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo utoro, utapeli na kuchezea Teknolojia na Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa lengo la kuiba makusanyo.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Mei 16, 2019 na Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustapher, baada ya baraza hilo kujadili tuhuma hizo.

Waliofukuzwa ni aliyekuwa ofisa mtendaji mtaa wa Jamhuri kata ya Ngamiani Kusini ambaye anadaiwa kuchezea mtandao na kujipatia fedha za makusanyo mbalimbali ya Serikali.

Mustapher amesema mtumishi huyo amekuwa akijihusisha na tuhuma za utapeli kwa wananchi anaowahudumia na kwamba baadhi ya malalamiko yapo kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi.

Mtumishi mwingine aliyefukuzwa alikuwa idara ya afya Kituo cha Afya Ngamiani anayetuhumiwa kwa utoro, huku akijua sheria inamtaka mtumishi asiyehudhuria kazini siku tano mfululizo kuchukuliwa hatua lakini yeye hakuripoti kazini kuanzia Juni 12 hadi Agosti 6, 2018.

Wengine ni aliyekuwa mtendaji mtaa wa Old Nguvumali;  wawili wa idara ya afya; na watano ambao ni watendaji.

Aliyeshushwa mshahara ambaye naye tuhuma zake zinaangukia katika moja ya makosa hayo matatu ni mtendaji wa mtaa Kwanjekanyota jijini Tanga.

Akifafanua kuhusiana na tuhuma hizo, meya huyo amesema adhabu zimetolewa baada ya kuketi kamati ya maadili iliyomhoji kila mmoja ikafuatia kamati ya fedha kabla ya kufikishwa baraza la madiwani na kwamba, vikao vyote vimewakuta na hatia.

 


Advertisement