Barrick kuinunua Acacia kumaliza mgogoro na Serikali ya Tanzania

Muktasari:

Kutokana na mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili baina ya Serikali na Acacia, kampuni ya Barrick Gold Corporation imetoa ombi la kununua hisa zote za Acacia ili kuwa na sauti moja kwenye mazungumzo yanayoendelea.

Dar es Salaam. Kutokana na mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili baina ya Serikali na Acacia, kampuni ya Barrick Gold Corporation imetoa ombi la kununua hisa zote za Acacia ili kuwa na sauti moja kwenye mazungumzo yanayoendelea.

Taarifa iliyotolewa juzi na Makamu wa Rais wa Uhusiano wa Umma wa Barrick, Deni Nicoski ilisema kampuni hiyo imekutana na menejimenti ya Acacia na kuwasilisha pendekezo hilo la kununua asilimia 35 ya hisa ambazo haizimiliki.

“Barrick imekuwa na majadiliano na Serikali ya Tanzania kwa miaka miwili iliyopita kutafuta suluhu ya kudumu kwenye mgogoro wake na Acacia ili uzalishaji uendelee kama kawaida na kurudisha uhusiano uliokuwapo zamani. Hata hivyo, Serikali haikuwa tayari kuzungumza chochote na Acacia,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Ili kufanikisha ununuzi wa Acacia inayokadiriwa kuwa na thamani ya Dola787 milioni za Marekani, Barrick imependekeza kubadilishana hisa zake na wamiliki wachache wanaobaki Acacia.

Katika thamani hiyo, tathmini zinaonyesha kuwa asilimia 35 ya wanahisa wanaobaki Acacia wanamiliki Dola285 milioni za Marekani. Endapo ombi hilo litakubaliwa, wanahisa waliobaki Acacia watakuwa sehemu ya wanahisa wa Barrick, hivyo mazungumzo yaliyopo kati ya Serikali na kanuni hiyo yataendelea kama kawaida na kutekelezwa kwa wakati.

Kutokana na taarifa hiyo ya Barrick, jana Acacia iliwataarifu wanahisa wake kuwa imepokea mrejesho wa mazungumzo yanayoendelea kati ya Barrick na Serikali ya Tanzania kuhusu mgogoro uliopo na kwa mara nyingine haijashirikishwa kwenye majadiliano hayo.

“Barrick imetupa nyaraka tofauti za makubaliano ambayo bado hayajaridhiwa. Vilevile imetupa barua ya Mei 19, 2019 kutoka kwa kaimu mwenyekiti wa kamati ya majadiliano iliyotumwa kwa kampuni tanzu zetu tatu za Bulyanhulu, North Mara na Pangea ikisema haitatafuta mwafaka wa mgogoro uliopo kama Acacia ni sehemu ya wahusika na itaridhia mapendekezo yaliyopo endapo itajiridhisha na mabadiliko ya kiuongozi na wanahisa wa kampuni hii,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Acacia. Pamoja na mrejesho huo, Acacia imewajuza wanahisa wake kupokea ombi la kununuliwa na Barrick kwa Pauni 1.47 za Uingereza kwa kila hisa zitakazofanywa kuwa sehemu ya wamiliki wa kampuni ya Barrick.

Msemaji mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas, alisema Serikali imeikataa Acacia na kwamba majadiliano ya mwisho yamemalizika na Serikali ipo tayari kutekeleza makubaliano isipokuwa haitafanya kazi na Acacia kutokana na makosa waliyoyafanya.