Barrick yamalizana na Acacia

Muktasari:

  • Ombi la Barrick lililotolewa Mei kutaka kununua asilimia 36.1 ya hisa za Acacia isizomiliki sasa limefanyiwa kazi na utekelezaji wake utafanyika muda wowote kuanzia sasa.

Dar es Salaam. Kampuni ya Barrick imekubali kuongeza bei ya kununua hisa na mali zote za Acacia inayomiliki migodi mitatu nchini.

Barick ilitangaza mpango wake wa kununua hisa za Acacia Mei mwaka huu. Katika mpango huo unaolenga kubadilisha hisa za Barrick kwa zile za Acacia ili kuwaingiza wanahisa wa Acacia kumiliki hisa za Barrick, ulipendekeza kwa kila hisa 1,000 za Acacia wapate hisa 153 za Barrick sawa na uwiano wa 0.153.

Wanahisa wa Acacia waligomea mpango huo wakisema hisa zao zina thamani kubwa ambayo ni kati ya Pauni 2.71 hadi Pauni 2.81 za Uingereza tofauti na inavyofikiri Barrick.

Baada ya msimamo huo, Barrick leo, Julai 19, 2019 imeongeza bei na kusema ipo tayari kutoa hisa 168 kwa kila hisa 1,000 za Acacia ambao ni sawa na uwiano wa 0.168. kwa tathmini hiyo mpya, Barrick italipa Pauni 2.32 kwa kila hisa ya Acacia.

“Bodi za wakurugenzi wa Barrick na Acacia zimepata muafaka wa kununua hisa za Acacia ambazo hazikuwa zinamilikiwa na Barrick. Barrack itatoa hisa zake kwauwiano wa 0.168 na kuwalipa gawio kwenye kila utafiti unaoendelea,” inasomeka taarifa ya Barrick iliyotolewa leo.

Kwenye ombi lililotolewa Mei, Barrick ilipendekeza kununua hisa za Acacia kwa bei pungufu kwa asilimia nane ya iliyotolewa sasa, Pauni 2.32.

Barrack ilikuwa inamilikia asilimia 63.9 ya hisa za Acacia na asilimia 36.1 ambazo ni sawa na hisa 410,085,499 zilikuwa zinamilikiwa na wanahisa wengine.

Kwa makubaliano haya mapya, Barrick itapaswa kulipa Acacia jumla ya Dola 1.186 bilioni za Marekani zikiwamo Dola 428 milioni ambazo ni thamani ya hisa.

Licha ya migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu inayomiliki nchini, Acacia inaendelea na utafiti huko Nyanzaga. Acacia pia inafanya utafiti nchini Kenya, Mali na Burkina Faso.

Kutokana na makubaliano baina ya kampuni hizo mbili, mazungumzo yaliyokuwa yamekwama kati ya Serikali ya Tanzania na Barrick sasa yataendelea.

Miaka miwili iliyopita, Tanzania iliipiga Acacia faini ya Dola 190 bilioni kwa madai ya kukwepa kodi na kukiuka miiko ya biashara na ikazuia usafirishaji wa mchanga wa madini  suala lililolalamikiwa na kampuni hiyo kuwa linapunguza mapato yake.

Kwa kuwa Acacia ni kampuni tanzu ya Barrick, Serikali ilikuwa inaongea na Barrick lakini Acacia ikawa inakataa kutekeleza maazimio yanayoafikiwa kikwazo ambacho sasa kinaondolewa.