VIDEO: Bashe aichambua bajeti ya Serikali 2019/2020

Muktasari:

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe ameichambua bajeti kuu ya Serikali mwaka 2019/2020 kwa maelezo kuwa bajeti za wizara tatu zinazochangia zaidi ya asilimia 30 ya pato la Taifa  zimetengewa fedha kidogo

 


Dodoma. Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe ameichambua bajeti ya Serikali ya mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni kwa kueleza jinsi wizara tatu zinazochangia asilimia zaidi ya 30 ya Pato la Taifa zilivyotengewa fedha kidogo za maendeleo.

Huku akichambua mfumo mzuri wa ufanyaji biashara ili kuondoa malalamiko na nchi kupata mapato zaidi, Bashe amesema ni lazima kuunganisha uzalishaji wa malighafi na ukuaji wa viwanda.

Mbunge huyo ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 18, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti kuu ya Serikali huku akizitaja wizara hizo tatu kuwa ni; Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Viwanda na Biashara.

Bajeti ya Kilimo mwaka 2019/2020 ni Sh253.85 bilioni zikiwemo Sh143.57 bilioni za maendeleo; Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sh64.91 bilioni (Sh17.69 bilioni ni za maendeleo) na Wizara ya Viwanda na Biashara Sh100.38 bilioni (Sh51.5 bilioni za Maendeleo). Fedha za maendeleo katika bajeti ya 2019/2020 ni Sh12.25 trilioni.

“Ukichukua bajeti yote ya maendeleo ya Sh12 trilioni na kuangalia kiasi kilichotengwa katika sekta ya kilimo na mifugo utabaini ni ujumla ni Sh61 bilioni sawa na asilimia 1.3 ya fedha zote za maendeleo. Kwa hali hii hatuwezi kupiga hatua.”

“Sisi tunauza mazao ya kilimo, tumbaku imeshuka kutoka tani 1.2 milioni hadi  tani 50,000; korosho 2016/17 ilikuwa tani 265,000 na 2018/19 ni tani 224,000; mkonge tani 36,000 hadi tani 15,000; chai kutoka tani 26,000 tunakwenda tani 19,000; sukari kutoka tani 330,000 tunaenda tani 327,000; pareto kutoka tani 2,150 hadi tani 1,800,” amesema Bashe.

Bashe amesema licha ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupangiwa kukusanya Sh1.7 trilioni huenda wakashindwa na watendaji kutumbuliwa, akisisitiza kuwa ili kodi ikusanywe lazima kuwe na uzalishaji, kufanya biashara.

Amesema kutokana na uwekezaji kushuka katika sekta mbalimbali ushuru wa bidhaa na kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) vitashuka.

“Rais (John Magufuli) wakati akizungumza na wafanyabiashara alisema kodi za ndani zinashuka ambazo zipo sambamba na biashara. Kodi za ndani ni VAT, kodi ya mshahara na ushuru wa bidhaa. Kama hatutaweka utaratibu mzuri  na kuunganisha biashara hatuwezi kutoka,” amesema Bashe.

Amemshauri Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kukutana na Waziri wa Viwanda na Biashara kufanya mabadiliko ya sheria za taasisi mbalimbali za Serikali ili kuunganisha ufanyaji  biashara.

“Mfano mtu anayetaka kusajili biashara anakwenda sehemu inaitwa Brela (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni), chukueni sheria ya Brela na hizi taasisi zote mziingize ndani ya Brela ili mtu anapoingia kusajili biashara na kuchukua leseni anakutana na kila kitu ndani na akitoka anakwenda kufanya biashara yake,” amesema Bashe.