Bashe azungumzia uteuzi wake

Muktasari:

  • Leo Jumapili Julai 21, 2019, Rais wa Tanzania, John Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri kwa kuteua waziri na naibu waziri huku akimweka kando Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.

Dar es Salaam. Hussein Bashe  amemshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kumteua kuwa naibu waziri wa kilimo huku akiahidi kwenda kutoa mawazo mapya ndani ya wizara hiyo inayochangia asilimia 28 ya pato la taifa (GDP).

Bashe ametoa kauli hiyo leo Jumapili Julai 21, 2019 alipokuwa akizungumza na Mwananchi saa chache kupita tangu taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania ilipotoka na kuelezea uteuzi huo.

“Mimi niseme tu kwanza nimshukuru Rais kwa imani yake kwangu ambayo amenipa, kwa hiyo jukumu langu nimepewa kwenda kumsaidia waziri (wa kilimo, Japhet Hasunga) kwenda kuhakikisha tunafikia malengo na matamanio ya Watanzania,” amesema Bashe ambaye ni mbunge wa Nzega Mjini

Bashe amesema, “Hii ndio sekta iliyoajili Watanzania wengi, inaendesha uchumi wa nchini inachangia 28 ya GDP na asilimia 70 ya ajira lakini ina changamoto nyingi, nina amini katika ushirikiano tutafanikiwa.”

Katika taarifa hiyo ya uteuzi, Bashe anakwenda kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Innocent Bashungwa ambaye aliteuliwa kuwa waziri wa viwanda na biashara.

Pia, Rais Magufuli amemtua George Simbachawene kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira akichukua nafasi ya Januari Makamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Uteuzi huo wa leo Jumapili, umemhusu pia Balozi Martin Lumbanga ambaye ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).