Bashiru: Mjadala Katiba mpya ni demokrasia

Saturday April 20 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema mjadala kuhusu Katiba mpya ulioibuka bungeni jijini Dodoma wiki hii ni afya ya demokrasia.

Amesema mjadala huo unafungua fursa ya malumbano ya hoja kwa hoja kuhusiana na suala hilo, na ni mawanda mapana ya demokrasia.

Kauli ya Dk Bashiru imekuja baada ya baadhi ya wabunge wa upinzani Jumatano, Aprili 17, wakiwa bungeni kutumia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 kudai Katiba mpya kwa maelezo kuwa chama hicho tawala kiliwaahidi Watanzania wakati kikiomba ridhaa ya kuwaongoza.

Madai hayo yaliibuka wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ya 2019/2020 na aliyeanzisha hoja hiyo alikuwa mbunge wa viti maalumu (Chadema), Salome Makamba baada ya kushika shilingi ya waziri, akitaka majibu ya Serikali ni lini itaendeleza mchakato wa Katiba mpya.

Hoja yake iliungwa mkono na hivyo kutolewa fursa ya kuchangiwa. Wakati ikiungwa mkono na wenzake wa upinzani, wabunge wa CCM walipinga wakikumbushia jinsi vyama vya upinzani vilivyosusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba pamoja na kuipinga Katiba Inayopendekezwa kwa madai kuwa imechakachuliwa.

Dk Bashiru akizungumzia hilo, alisema, “ninafuatilia mijadala inayoendelea bungeni na wanavyojadili kuhusu Katiba mpya, hoja kwa hoja, malumbano bila kutukanana ndiyo afya ya demokrasia, nachelea kujibu kuhusu suala hilo kwa sababu nitaufunga mjadala huo.”

Alisema kinachoulizwa bungeni kinajibiwa bungeni kwenye maswali na majibu na ndiyo kazi ya Bunge.

Bunge la Katiba lilikamilisha kazi yake ya kuandika Katiba mpya kwa upigaji kura za kupitisha Rasimu ya Katiba ambayo ilitakiwa ipitishwe kwa kura ya maoni ya theluthi mbili ya kura kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini mchakato huo ulisimama kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Katika hoja yake, Salome alisema kuwa licha ya Rais John Magufuli kunukuliwa akisema kuwa suala la Katiba mpya siyo kipaumbele chake kwa sasa, limo katika Ilani ya CCM.

“Lakini ukurasa wa 206 na 207 wa Ilani ya CCM inasema wazi, ‘Ili kuendeleza utawala bora, demokrasia na uwajibikaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo CCM itahakikisha inatekeleza yafuatayo; (g) kukamilisha mchakato wa kutunga Katiba mpya na kuanza kuutekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema mbunge huyo.

Mbunge huyo aliitaka Serikali kuwaeleza wananchi ni lini watapata Katiba mpya.

Akijibu hoja hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi alisema, “Katiba ni dira na ndio mwongozo ila mchakato wa Katiba utaendelea kulingana na mazingira na mahitaji yatakavyoruhusu.”

Salome hakuridhika na maelezo ya Profesa Kilangi, na badala yake alishika shilingi kuruhusu wabunge kuchangia hoja hiyo.

Katika mchango wake, mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu alisema ili kulinda utulivu na amani suala hilo limalizwe.

Naye mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji alisema anashangazwa na CCM wasivyotaka kuendeleza mchakato huo wakati walifanya sherehe na kupeana nishani wakati wakipitisha Katiba Inayopendekezwa.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Susan Lyimo alichangia madai hayo kwa kusema kuwa, “Dk Bashiru (Ally, katibu mkuu wa CCM) anapita sehemu mbalimbali akisema wanatekeleza ilani ya chama hicho, ni kama mnawalaghai wananchi na mnasema tunaishi katika Katiba ni katiba ipi hiyo?”

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alisema kama suala la Katiba mpya haliwezekani, Serikali ifanye marekebisho ya Katiba na sheria ili ipatikane tume huru ya uchaguzi.

Advertisement