Bashiru amuonya Nkamia urais CCM

Muktasari:

  • Akizungumza baadaye na Mwananchi kuhusu kauli ya katibu mkuu huyo wa CCM, Nkamia alisema “unajua mimi ni mtoto niliyelelewa na kufunzwa katika maadili ya kuheshimu wakubwa na wazazi…. siwezi kukiuka, nimetii maelekezo ya wazazi. Mimi ni kijana mwelewa wazazi wamesema niache, mimi nimeacha.”

Dodoma. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amemuonya mbunge wa Chemba, Juma Nkamia kuachana na kampeni ya kutaka muda wa urais kuongezwa akisema ndani ya chama hicho hakuna usultani.

“Yupo mwingine hapa, (mbunge wa Chemba, Juma Nkamia), hapana usifanye hivyo, siyo msimamo wa CCM. Hatutaki kuwa na viongozi masultani ndani ya CCM ama ndani ya Serikali ya CCM ama ndani ya CCM yenyewe,” alisema Dk Bashiru jana alipokuwa akizindua mkakati wa kukomaza demokrasia katika ngazi ya mashina ulioandaliwa na CCM Mkoa wa Dodoma mjini hapa.

Baada ya Dk Bashiru kutoa onyo hilo, Nkamia ambaye alikuwepo katika uzinduzi huo alisimama na kuinama ikiwa ni ishara ya kuonyesha utiifu.

Akizungumza baadaye na Mwananchi kuhusu kauli ya katibu mkuu huyo wa CCM, Nkamia alisema “unajua mimi ni mtoto niliyelelewa na kufunzwa katika maadili ya kuheshimu wakubwa na wazazi…. siwezi kukiuka, nimetii maelekezo ya wazazi. Mimi ni kijana mwelewa wazazi wamesema niache, mimi nimeacha.”

Nkamia, amekuwa akijitokeza mara kwa mara kutaka muda wa urais uongezwe ili Rais John Magufuli akae muda mrefu zaidi ya ule unaotambulika kikatiba wa miaka mitano katika kipindi kimoja au miaka kumi vipindi viwili.

Kwa mujibu wa Katiba, Rais aliyepo madarakani ukomo wake ni vipindi viwili yaani miaka kumi.

Katika hoja yake ya kutaka muda huo uongezwe, kwa nyakati tofauti, Nkamia amewahi kuzungumzia kutaka kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili sheria ibadilishwe Rais wa nchi awe anatawala kwa miaka saba badala ya mitano ya sasa.

Lakini, jana Dk Bashiru hakutaka kuacha suala hilo lipite bila kulizungumzia.

“Dk John Magufuli atamaliza awamu yake ya kwanza ya miaka mitano na ataomba ridhaa ndani ya chama chake kwa kufuata Katiba. Nina uhakika kuwa mtampa kura nyingi za kutosha,” alisema Bashiru.

Alisema atafanya hivyo kama alivyong’atuka Mwalimu Julius Nyerere na marais wengine na kwamba watampata rais bora baada ya Magufuli kumaliza kipindi chake cha uongozi.

“Napenda kuhitimisha mjadala usio rasmi unaoendelea kuhusu hatima ya nchi hii baada ya John Pombe Magufuli. Hatima ya nchi hii iko mikononi mwa wana-CCM,” alisema.

Alisema wana-CCM hasa wanawake wanambegu za kuzalisha viongozi bora na kazi ya kuhakikisha kunakuwa na viongozi bora, siyo kwa Magufuli kukaa muda mrefu madarakani ama kubadilisha utaratibu ulipo, bali kuimarisha chama chao.

Alisema mkakati huo unalenga katika kuhakikisha kunakuwa na viongozi bora wakati wote.

Awasha moto kwa viongozi

Dk Bashiru aliwasha moto kwa kuwataja viongozi ambao hawana uhusiano mzuri na viongozi wengine katika maeneo yao akimtaja Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Mbali na viongozi hao, Dk Bashiru amemtaja waziri mmoja kijana anayeongoza taasisi mbalimbali akisema kuwa hana adabu.

“Hasa kauli kwa watu walio chini yake anawaambia ‘we mbona mwizi’ wakati hana ushahidi, pia (huyo waziri) anasema ‘we mbona huna elimu, we mbona mzee’. Yeye (waziri) kateuliwa na Rais na anawafokea ambao wameteuliwa kama yeye ambao wote wanamtumikia Rais,” alisema.

Mtendaji huyo mkuu wa chama tawala alitoa kauli hiyo kipindi ambacho kumekuwapo na hali ya kutoelewana kwa baadhi ya watendaji wa Serikali wa wilaya na mikoa hadi kufikia hatua ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwatuma mawaziri wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo kwenda kutatua mgogoro wa kiuongozi wa wilaya na Mkoa wa Kilimanjaro.

Februari 20, Majaliwa aliwaonya mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Sada Malunde na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Wende Ng’ahara kuwa wasipomaliza tofauti zao atamshauri Rais afanye uamuzi mwingine.

Dk Bashiru akunjua makucha

Katika maelezo yake jana, Dk Bashiru alisema amemwagiza mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Godwin Nkanwa kwenda wilayani Chemba kutafuta sababu za msingi kwa nini mbunge wa Chemba, Juma Nkamia; mkurugenzi mtendaji wa halmashauri, Dk Semistatius Mashimba na mkuu wa Wilaya, Simon Odunga hawana sauti moja.

“Na katibu wangu wa chama pale (Chemba) nakuondoa leo, huwezi kumudu kazi ya kuongoza wilaya mpya na ndani ya wiki moja mwenyekiti (wa CCM) uwe umeniletea taarifa. Kulikuwa na tatizo Dodoma mjini nikakutuma ukafanya kazi hiyo na tatizo hilo limekwisha,” alisema.

Alisema tatizo la viongozi kutoelewana na kuwa na uhusiano mbaya pia lipo wilayani Siha, Kilimanjaro; Kyela (Mbeya) na kwamba Dar es Salaam sasa imetulia kama maji mtungini.

“Kuna tatizo Arusha hasa mkuu wa Mkoa wa Arusha (Mrisho Gambo). Mara pametulia lakini kwa wastani. Kwa ujumla ujumbe wa kujenga mahusiano mema umepokelewa vizuri na hali ni nzuri.”

Alisema kinachosumbua ni watu kutofuata utaratibu na kudharauliana akisema, “maana nasikia pale Chemba mkurugenzi na mkuu wa wilaya wanatunishiana misuli.”

“Nani mwenye elimu zaidi kuliko mwingine, nani mwenye madaraka zaidi kuliko mwingine. Watatoka wote. Kabla hawajatoka wamsikilize mwenyekiti wa chama yeye ndiye mkuu wa chama katika mkoa huu.”

Alimwagiza Mkanwa kuwa kiongozi atakayeshindwa kumsikiliza ampelekee jina lake ambalo atalipeleka kwa mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Magufuli.

Dk Bashiru pia alisema kuna ugonjwa umezuka wa kufukuzana badala ya kukosoana na kuonyana na kwamba hatua ya kumfukuza kiongozi ni ya mwisho.

“Kondoa nimesikia habari huko. Msiwafukuze watendaji bila kujiridhisha faida na hasara zake. Tunachotaka ni kujenga mahusiano bora. Kufukuza fukuza nako hakujengi sana,” alisema.

Alama za vyama vya siasa

Akizungumzia alama ya vyama vya siasa, mtendaji huyo wa CCM alisema, “sio tu kuheshimu alama za chama chetu, bali kuheshimu pia alama za vyama vingine. Hatutarajii katika CCM mwanachama yeyote kuchoma bendera ya chama kingine, kubeza alama ya chama kingine kwa sababu vyama vyote vipo kwa mujibu wa sheria.”

Alisema kuna watu wanaojiita wafuasi wa vyama fulani ambao wameanza kuchoma bendera ya chama kingine, kuparamia majumba na kupaka rangi, akisema ni kosa la jinai.

“Lakini CCM tuziagize serikali zetu kusimamia sheria. Tusiruhusu uholela wala uhuni katika siasa za nchi yetu. Matarajio yangu ni kwamba upuuzi huo utakoma mara moja.”

Aliongeza kuwa, “kuna wajibu wa kuvipa ulinzi vyama vyote vilivyosajiliwa kisheria. Lakini tunawajibu wa kuwa mfano bora katika kuendesha siasa zetu kwa misingi ya kidemokrasia.”