Bei ya unga wa sembe yapanda, Serikali yatoa sababu

Dar/mikoani. Bei ya unga imepanda katika maeneo mbalimbali nchini, jambo ambalo limesababishwa na kupanda kwa bei ya mahindi ambayo ndiyo chakula kikuu cha Watanzania walio wengi.

Ufuatiliaji wa bei ya unga uliofanywa na waandishi wetu katika maeneo mbalimbali nchini jana Jumapili kuanzia saa nne asubuhi hadi saa 10 alasiri, umeonyesha kuna ongezeko ambalo Serikali imelithibitisha na kueleza kuwa limetokana na ukame ambao umesababisha maeneo yanayotegemea mvua za vuli kushindwa kuvuna mahindi msimu huu.

Waandishi wetu walipotembelea maeneo ya Kinondoni, Tegeta na Kunduchi, Dar es Salaam walikuta kilo ya unga ikiuzwa kwa wastani wa Sh1,200 kutoka wastani wa Sh900. Bahari Beach kilo tano za walikuta zikiuzwa Sh6,000 kutoka wastani wa Sh4,000.

Huko Mtwara, mwandishi wetu alibaini kilo moja kuuzwa kwa wastani wa Sh1,000 na 1,200 kutoka wastani wa Sh800 na katika Mji wa Mugumu Wilaya ya Serengeti, bei hadi hiyo alasiri ya jana, kilo ya unga ilikuwa ikiuzwa kwa wastani wa Sh1,200 kutoka wastani wa Sh900 huku Arusha ikitoka kwenye wastani wa Sh900 hadi wastani wa Sh1,100.

Mjini Moshi, bei ya mahindi katika Soko la Mbuyuni mchuuzi Anna Joseph alisema hadi jana mchana, mfuko wa kilo 25 ulikuwa umepanda kutoka Sh21,000 hadi Sh25,000.

Jijini Mbeya hadi jioni, bei ya kilo moja ilikuwa Sh1,200 kutoka Sh1,000. Katika Mji Mdogo wa Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara bei hadi jioni ilikuwa Sh1,000 kutoka Sh800.

Akizungumzia hali hiyo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema ni ya kawaida kwa sababu upatikanaji wa mahindi umepungua kutokana na hali ya ukame.

“Maeneo mengi ambayo yalikuwa tayari wavune mahindi yale ya vuli, mwaka huu hayapo, yamekauka kwa sababu ya ukame. Kwa hiyo, matokeo yake mahindi yamepanda bei maeneo mengi,” alisema Waziri Hasunga.

Alisema katika maeneo mengi mahindi yamepungua na kusababisha bei kupanda. Alisema katika baadhi ya maeneo, gunia la mahindi linauzwa Sh45,000, Sh50,000 na Sh55,000 huku akiongeza kuwa bei hiyo inaweza kufika Sh100,000.

Alipoulizwa kama Serikali itaingilia kati suala la bei alisema, “hatuwezi, tunaliangalia tu. Kuna wakati wananchi walikuwa wanalalamika kwamba bei ya mahindi iko chini, sasa ni kipindi ambacho bei imekuwa nzuri,” alisema.

Ripoti ya hali ya uchumi ya Benki Kuu (BoT) iliyotolewa Machi inaonyesha bei ya jumla ya mahindi katika mikoa mbalimbali iliongezeka Februari ikilinganishwa na mwezi uliotangulia.

Ripoti hiyo inaonyesha wastani wa bei ya jumla ya mahindi (kilo 100) ilikuwa juu kwa asilimia 3.7 na kufikia Sh50,811.6 Februari kutoka Sh49,011.1 iliyorekodiwa Januari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kila mwezi, bei ya mahindi ya Februari 2018 ilikuwa juu kwa asilimia 4.7 kuliko Sh48,530.1 kwa kilo 100 zilizoripotiwa Februari 2018. Hata hivyo, BoT haikufafanua sababu za ongezeko hilo.

Licha ya bei ya mahindi kuongezeka, BoT imeeleza chakula kipo cha kutosha katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na mavuno mazuri katika msimu wa mwaka 2017/18.

Ripoti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ya Aprili 8 inaonyesha kiwango cha chini cha bei ya jumla kwa kilo 100 katika Mkoa wa Dar es Salaam kilikuwa Sh54,000 ambacho kiko juu kikilinganishwa Sh46,000 kilichorekodiwa Desemba mwaka jana.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Kilimo, uzalishaji wa mahindi kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 ulikuwa tani milioni 6.2 kutoka tani milioni 6.6 zilizorekodiwa mwaka uliotangulia.

Imeandikwa na Peter Elias (Dar), Janeth Joseph (Moshi), Joseph Lyimo (Manyara), Haika Kimaro (Mtwara), Anthony Mayunga (Serengeti)