Benki ya Azania yajivunia kuichukua Benki M

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Charles Itembe akizungumza na waandishi jijini Dar es Salaam, kuhusu ubora wa huduma za benki  hiyo baada ya kununua Benki M. Picha na Salim Shao

Muktasari:

 

  • Benki ya Azania imetangaza kuwa siku 40 zijazao matawi benki M yaliyokuwa yamefungwa tangu Desemba 21 yatakuwa wazi huku ikijivunia kuichukua benki hiyo kwa kile inachoeleza imeongeza mtaji wake na kupanua wigo wa huduma.

Dar es Salaam. Benki ya Azania (ABL) imesema kuunganishwa kwake na benki M kumeiongozea mtaji kutoka Sh64 bilioni hadi Sh184 bilioni huku jedwali la mizania (Balance sheet) likiongezeka kutoka Sh500 bilioni hadi zaidi ya Sh1 trilioni.

Benki hiyo imesema siku 40 zijazo milango ya matawi ya iliyokuwa benki hiyo yatakuwa wazi kuwahudumia wateja wote wakiwamo wa Azania na wateja wa iliyokuwa benki M watapata huduma tawi lolote la Azania.

Mkurugenzi mtendaji wa benki ya Azania Charles Itembe, leo Jumatano Machi 20, 2019 amewaeleza waandishi wa habari kuanzia Machi 15 mwaka huu ABL ilikamilisha rasmi mchakato kuhamisha mali na madeni ya iliyokuwa benki M.

“Desemba 21 ulifanyika uamuzi wa ABL kupewa benki M na wanahisa walikubali kuongeza mtaji ili kuifanya Azania kuwa imara zaidi, uamuzi huo umeifanya Azania sasa kuwa na matawi 22 tofauti na awali ilipokuwa na matawi 19,” amesema Itembe.

Amesema benki hiyo imerithi kitabu cha mali na madeni ambavyo vina thamani ya zaidi ya Sh800 bilioni na wafanyakazi 116 wa benki M ambao mikataba yao ilikuwa haijaisha wataendelea kufanya kazi ABL.

Ameongeza kuwa uwiano wa mikopo chechefu katika ABL mpaka mwishoni mwa mwaka jana ilikuwa asilimia 6 huku benki M ikiwa asilimia 40, hivyo kwa kuchukuliwa uwiano wa mikopo chechefu Azania utaongezeka lakini kuna mipango ya kupunguza kiwango hicho.