Benki ya Dunia yaiahidi Tanzania mkopo wa Sh4 trilioni

Muktasari:

 

  • Benki ya Dunia (WB) imesema itaendelea kutoa misaada na mikopo ya masharti nafuu kwa Tanzania kwa mwaka 2019/20

Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imeahidi kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu na msaada wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.7 sawa na takriban Sh4 trilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.

Ahadi hiyo imetolewa mjini Washington nchini Marekani na Makamu wa Rais wa Benki hiyo anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Hafez Ghanem, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano cha wizara ya fedha na mipango imemnukuu Ghanem ambaye amemhakikishia Rais wa Tanzania, John Magufuli kwamba uhusiano kati ya Serikali na Benki yake bado uko imara na WB iko tayari kushirikiana na Tanzania ili iweze kufikia maendeleo yanayotarajiwa.

Miongoni mwa miradi itakayonufaika na mkopo na msaada huo ni mpango wa elimu ambapo benki hiyo imeongeza ufadhili kutoka Dola milioni 300 hadi Dola milioni 400 na mradi wa kusaidia kaya masikini kupitia Tasaf ambapo benki hiyo imeamua kuongeza kiwango cha fedha kutoka Dola milioni 300 hadi kufikia Dola milioni 450.

Kiasi kingine cha fedha kitatumika kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za miundombinu ya barabara, maji, Tehama, afya, kilimo, hifadhi ya jamii, nishati, utawala bora, lishe, sekta ya fedha, biashara, mazingira na maliasili pamoja na maji.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri Mpango ameishukuru benki hiyo namna inavyoisaidia nchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambapo hadi sasa benki hiyo imefadhili miradi 21 ya maendeleo kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 4.8, sawa na takriban Sh11 trilioni.

Ameahidi Serikali ya Tanzania itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa masuala mbalimbali na kuiomba benki hiyo iendelee kuisaidia nchi ili iweze kufikia maendeleo yaliyokusudiwa ikiwemo kuondoa umasikini wa wananchi.

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri Mpango pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga, upo mjini Washington D.C kuhudhuria mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), taasisi ambazo Serikali ina hisa.